Ewura yashusha tena bei ya mafuta

Mkurugenzi Mtendaji wa EWURA, Haruna Masebu.

MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), imeshusha bei ya mafuta kuanzia leo.Kwa hatua hiyo, bei ya ukomo ya petroli kwa Mkoa wa Dar es Salaam sasa itakuwa Sh2,070, huku dizeli ikiwa Sh1,999 na mafuta ya taa Sh1,980. Bei ya ukomo wa bidhaa hiyo itatofautiana kulingana na umbali wa maeneo.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Haruna Masebu alisema hiyo ni kutokana na kushuka kwa bei ya bidhaa hiyo katika soko la dunia.Alisema ikilinganishwa na bei ya zamani, petroli imeshuka kwa Sh44.55 sawa na asilimia 2.11 huku dizeli ikishuka kwa Sh31.99 sawa na asilimia 1.57 na mafuta ya taa yakishuka kwa Sh25.62 sawa na asilimia 1.28.Mnamo Agosti 2, Ewura, ilishusha bei ya mafuta.

Petroli ilishuka kwa Sh202.37 kwa lita ambayo ilikuwa ni sawa na asimilia 9.17, dizeli kwa Sh173.49 sawa na asilimia 8.32 na mafuta ya taa kwa 181.37, sawa na asilimia 8.70 hali iliyosababisha vurugu na uhaba wa bidhaa hiyo.

Lakini, siku 11 baada ya kushusha bei hiyo, Ewura ilipandisha tena bei ya mafuta kutokana na kile ilichodai kuwa ni kupanda bei katika soko la dunia na kushuka kwa thamani ya shilingi ya Tanzania na kusababisha Bodi ya mamlaka hiyo kubanwa na Baraza la Mawaziri.

Jana, Masebu akitangaza nafuu hiyo ya bei ya mafuta, alisisitiza: “ Tutaendelea kukokotoa bei za bidhaa za mafuta kila baada ya wiki mbili, hiyo itatokana na mabadiliko ya bei ya bidhaa za mafuta katika soko la dunia na kushuka kwa thamani ya shilingi ya Tanzania ikilinganishwa na Dola ya Marekani.”

Alisema kwa mujibu wa Sheria ya Mafuta ya mwaka 2008, bei ya mafuta zitaendelea kupangwa na soko… “ Ewura itaendelea kuhamasisha ushindani kwa kutoa taarifa za bei kikomo za bidhaa za mafuta.” Alisema kampuni za mafuta ziko huru kuuza bidhaa za mafuta kwa bei ya ushindani ili mradi ziko chini ya bei ya kikomo.“Wafanyabiashara na wateja wakubaliane na bei zitak azopangwa na Ewura kwa kuwa bidhaa za mafuta zinabadilika mara kwa mara,” alisema.

Masebu alisema vituo vyote vya mafuta vinatakiwa kuchapisha bei ya bidhaa hiyo katika mabango yanayoonekana bayana na kuwataka wateja kununua mafuta katika vituo vinavyouza kwa bei ya chini ili kuhamasisha ushindani.
“Ni kosa kuuza mafuta bila kuweka mabango ya bei inayoonekana vizuri kwa wateja na adhabu itatolewa kwa kituo kitakachokiuka agizo hilo,” alisema Masebu.

Alisema wanunuzi wanashauriwa kudai stakabadhi ya malipo inayoonyesha jina la kituo, tarehe, aina ya mafuta yaliyonunuliwa na bei yake kwa lita.

“Stakabadhi hiyo ya malipo itatumika kama kidhibiti cha mnunuzi wa mafuta endapo kutajitokeza malalamiko ya ama kuuziwa mafuta kwa bei ya juu kuliko bei kikomo yenye kiwango cha ubora usiofaa,” alisema Masebu.

Bei kikomo kwa kanda Kwa mujibu wa jedwali la Ewura, bei ya petroli kwa Mkoa wa Arusha sasa ni Sh2,154, huku dizeli ikiwa Sh2,083 na mafuta ya taa Sh2,064.Mkoa wa Dodoma petroli itauzwa kwa Sh2,128, dizeli Sh2,058 na mafuta ya taa Sh2,038.Katika mkoa wa Mwanza petroli sasa ni Sh2,219 huku dizeli Sh2,149 na mafuta ya taa Sh2,130.Jedwali hilo la bei linaonyesha kwamba, bei kwa mkoa wa Mbeya petroli itauzwa kwa Sh2,176 huku dizeli ikiuzwa kwa Sh2,106 na mafuta ya taa kwa Sh2,087.Mkoa wa Kigoma petroli itauzwa kwa Sh2,301, dizeli Sh2,230 na mafuta ya taa Sh2,211.

Tetesi za vitishoMkurugenzi huyo alisema kuna tetesi za baadhi ya wamiliki wa vituo vya mafuta wanaotii maagizo ya Serikali kutishiwa na washindani wao. Alisema wamiliki hao wamekuwa wakiwatishia wenzao wanaopinga maagizo ya Serikali kwa kutaka waungane nao ili wawe na nguvu katika madai yao.

“Siwezi kuingia kwa undani kama nilivyosema hizi ni tetesi ambazo tunazifanyia kazi, ikibainika watakuwa wanatenda kosa na watachukuliwa hatua za kisheria,” alisema Masebu. Vituo vya mafuta vyafungiwa Mamlaka hiyo imevifunga vituo vitatu vya mafuta katika Mikoa ya Dar es Salaam, Iringa, Mwanza kutokana na kuvunja sheria.

Ofisa Uhusiano wa Ewura, Titus Kaguo alisema kwa Dar es Salaam Kituo cha mafuta cha Kobil kilichopo Kigamboni kimefungiwa kutokana na kuuza mafuta yaliyochakachuliwa. Alisema kituo hicho ambacho kilifungiwa Agosti 26, mwaka huu, kimepewa siku saba kujieleza kwa nini kisichukuliwe hatua za zaidi za kisheria kwa kosa hilo.

Kaguo alisema kituo kingine kilichofungiwa ni Hass Magu kilichopo Magu, Mwanza ambacho baada ya kufungiwa na Ewura kiliendelea kuuza mafuta.Kingine kilichofungiwa ni Mafinga Petrol Station ambacho uongozi wake uliwakataza wakaguzi wa Ewura kufanya kazi yao.

“Kwa hiyo ninataka kuwaeleza wananchi kwamba Ewura tupo kila mahali, tutawachukulia hatua wale wote wanaokiuka sheria,” alisema Kaguo.
CHANZO; Mwananchi