North Mara Watumia Bilioni 1.7 Kujenga Shule

Mama Salma Kikwete akishirikiana na viongozi wa Mkoa wa Mara na wale wa Wilaya ya Tarime na wahisani waliojenga Shule ya J.K. Nyerere

Mama Salma Kikwete akishirikiana na viongozi wa Mkoa wa Mara na wale wa Wilaya ya Tarime na wahisani waliojenga Shule ya J.K. Nyerere

Mgodi wa dhahabu wa North Mara uliopo wilayani Tarime umetumia kiasi cha shilingi bilioni 1.7 kwa ajili ya ujenzi wa shule ya Sekondari JK Nyerere pamoja na nyumba za walimu.

Ujenzi wa shule hiyo iliyopo kijiji cha Nyamwaga kinachopakana na mgodi huo umeenda sambamba na ununuzi wa samani za ofisi za walimu, madarasa na maabara.

Hayo yamebainishwa leo na Meneja wa Mgodi huo unaomilikiwa na kampuni ya ACACIA, Jimmy Ijumba wakati wa uzinduzi wa Shule hiyo uliofanywa na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete na kuhudhuriwa na viongozi wa Serikali, vyama mbalimbali vya siasa, wanafunzi na wananchi.

Ijumba alisema shule hiyo imejengwa kwa awamu ambapo kwasasa zimekamilika awamu mbili ambazo wigo wake ni madarasa nane, nyumba za walimu sita zenye vyumba vya kulala vitatu, stoo, jiko, bafu, tanki la maji pamoja na uzio, jengo la utawala, maktaba, maabara mbili, vyoo vya walimu na wanafunzi vyenye matundu 33.

Aidha Mgodi huo umenunua kompyuta za wanafunzi na walimu, photocopier machine, printer, projector na scanner kwa ajili ya shule hiyo.

Alifafanua kwamba ujenzi wa shule hiyo umekuwa ukitekelezwa kwa awamu kutokana na shule kuwa mpya kwani ina kidato cha kwanza na cha pili na kama majengo yote yangejengwa kwa wakati mmoja yangekosa matumizi.

“Awamu ya tatu ya ujenzi wa shule hii utatekelezwa mwakani kwa kuhusisha madarasa manne, bwalo la chakula na chumba cha kupumzikia wagonjwa”, alisema Ijumba.

Kwa upande wake Mama Kikwete aliipongeza kampuni ya ACACIA kwa kuchangia jitihada za Serikali za kuboresha elimu kwa watoto na kusema kuwa mfano huo unapaswa kuigwa na makampuni mengine hapa nchini.

Alisema njia pekee ya kupambana na ujinga, maradhi na umasikini ni kuwapeleka watoto shule kwani wao ndiyo tegemeo la wazazi, nguvu kazi na rasilimali ya taifa. Wakielimishwa watakuwa wanawatengenezea njia ya kujikomboa katika Nyanja za kijamii na kiuchumi na watakuwa msaada mkubwa kwa wazazi wao pindi watakapokuwa wazee.

Mama Kikwete alisisitiza, “Watoto wote wa kike na wa kiume wanahaki sawa ya kupata elimu kuanzia ya awali hadi ya juu, hakikisheni wanakwenda shule kusoma hasa masomo ya sayansi ambayo ni rahisi ukilinganisha na masomo mengine.

Tuachane na mila kandamizi za kufikiria kwamba watoto wa kike ni wa kuolewa tu na wa kiume ndiyo wa kusoma kama wazazi ni lazima tutambue kuwa kufanya hivyo ni kuvunja haki ya mtoto yatupasa kutambua kuwa ukimuelimisha mtoto wa kike unaelimisha jamii nzima,”.

Alitoa wito kwa kampuni ya ACACIA kuendelea kukamilisha mikataba waliyokubaliana na vijiji vinavyowazunguka na kuendelea kuisaidia jamii siyo ile tu inayoizunguka migodi bali hata iliyopo nje kulingana na mahitaji yao kwani Serikali inaamini rasilimali za Taifa zinapaswa kunufaisha wananchi wote bila kujali wapi zilipo.

“Rai yangu kwenu ni kuendelea kuimarisha mahusiano na wananchi ,mgodi uendelee kuwasaidia wachimbaji wadogowadogo kiteknolojia, ujenzi na vifaa, tafuteni namna nzuri zaidi ya kuwawezesha vijana na kina mama wanaotafuta dhahabu katika maeneo mnayohifadhi ambayo mmewaruhusu kufanya hivyo ili shughuli hiyo iwe rasmi na endelevu”, alihimiza.

Akisoma risala ya wananchi wa kijiji cha Nyamwaga Mwenyekiti wa kijiji hicho chenye wakazi zaidi ya 10,000 Getende Sagirai alisema kijijini hapo kuna shule moja ya sekongari ya JK Nyerere iliyojengwa na mgodi wa North Mara.

Sagirai alisema katika sekta ya elimu wanakabiliwa na upungufu wa walimu wa masomo ya sayansi, vifaa vya kufundishia na kujifunzia, maabara,umeme mashuleni,maji, vyombo vya usafiri, mabweni, mabwalo, kumbi za mikutano, viwanja vya michezo na ukosefu wa uzio katika maeneo ya shule pamoja na nyumba za walimu.

“Tunaushukuru uongozi wa kampuni ya ACACIA kwa mahusiano mema ambayo yanadhihirikashwa na vitu halisi visivyoweza kuhamishika wala kusahaulika na vizazi kwa vizazi vyote vya Nyamwaga.

Vitu hivi ni usambazaji wa maji safi kwa matumizi ya binadamu, ujenzi wa barabara, ukarabati wa shule ya msingi Nyamwaga unaoendelea, mradi wa Can educate unaofadhili watoto wanaotoka katika mazingira magumu ili wapate elimu, ujenzi shule ya sekondari, na ajira zinatolewa kwa vijana wa eneo hili katika mgodi”, alisema Mwenyekiti huyo wa Serikali ya kijiji.

Mradi wa ujenzi wa shule ya JK Nyerere ni moja kati ya miradi ya kijamii katika kijiji cha Nyamwaga inayotekelezwa kwa ufadhili wa mgodi kama ilivyoainishwa kwenye mkataba wa manufaa ya vijiji (VBIA) uliosainiwa kati ya mgodi na kijiji mwezi Februari 2012.

Miradi mingine ni ya sekta ya maji, afya, elimu, barabara za jamii, umeme na uchumi.