Rais Kikwete alikubali kuzindua Kituo hicho wakati wa mazungumzo kati yake na Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Umeme ya Symbion Power, Bwana Paul Hinks kwenye Hoteli ya JW Marriot Essex House, mjini New York, Marekani ambako Rais alikuwa anafanya ziara rasmi ya kikazi. Rais Kikwete alikiwekea Kituo hicho jiwe la msingi mwaka jana.
Katika mkutano huo, uliofanyika Septemba 29, 2015, Hinks alimweleza Rais Kikwete kuwa ujenzi wa Kituo hicho sasa umekamilika tayari kwa uzinduzi na hivyo kuongeza thamani kubwa kwenye eneo ambalo miaka ya nyuma lilikuwa gereji ya kutengenezea magari.
Kituo hicho cha JMK Park kimegharimu kiasi cha dola za Marekani milioni mbili na ni matokeo ya ushirikiano ya Kampuni ya Symbion Power ya Marekani, Klabu ya Soka la Ligi Kuu ya Uingereza ya Sunderland AFC na Taasisi ya Grasshopper Soccer.
Baada ya uzinduzi huo, Kituo hicho kitafunguliwa kwa umma kwa mara ya kwanza Jumamosi ya Oktoba 19, 2015, na hivyo kukiwezesha kuanza shughuli zake, shughuli kubwa ikiwa ni kulea watoto wa kike na kiume kwa kupitia michezo.
Kwa mujibu wa mipango ya sasa, Kituo hicho kitaanza kwa kutoa mafunzo ya michezo ya soka, mpira wa kikapu (basketball), netiboli, mpira wa wavu (volleyball) na mpira wa magongo (hockey), michezo ambayo viwanja vyake vya kisasa kabisa vimekamilika kujengwa.
Kuhusu soka, JMK Park kitaanza kutoa mafunzo ya mchezo huo kuanzia Januari 2016 kwa timu za watoto wa chini ya umri wa miaka 16 na miaka 14 na pia kitatoa mafunzo maalum kwa watoto wadogo zaidi wa kati ya miaka 10 na 11. Mafunzo hayo yatatolewa na makocha wenye weledi na uzoefu kabisa ambao watatolewa na Klabu ya Sunderland.
Kuhusu mpira wa kikapu, mafunzo yataanza kutolewa kwa watoto wa kiume wa kati ya miaka 12 na 15 kutoka shule 30 za msingi katika Mkoa wa Dar es Salaam ambazo zitaunda timu 30 zitakazoshiriki katika ligi ya mchezo huo kila mwaka. Mafunzo ya mchezo huo kwa ajili ya watoto wa kike, utaanza katika mwaka wa pili wa kufunguliwa kwa Kituo hicho. Kituo hicho ambacho kitafunguliwa kila siku kwa mwaka mzima pia kitatoa nafasi kwa watu wazima wapenzi wa michezo kukitumia kwa mujibu wa taratibu zitakazotangazwa baadaye na wahusika.