Maoni ya Wanawake Wajasiliamali Dhidi ya Serikali ya Rais Kikwete na Ijayo (2)

WATANZANIA wenye sifa za kupiga kura wanatarajia kupiga kura Oktoba 25 katika Uchaguzi Mkuu kuchagua viongozi ambao wataunda Serikali ya awamu ya tano na kuliongoza taifa kwa kipindi cha miaka 5 mfululizo. Yafuatayo ni maoni ya baadhi ya wanawake wajasiliamali walioshiriki Maonesho ya 39 ya Biashara Kimataifa (Sabasaba) katika Viwanja vya Mwalimu Julias Nyerere Barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam juu ya Serikali inayomaliza muda wake na ijayo.

Bi. Khadija Fussi mjasiliamali kutoka Muheza Tanga.

Bi. Khadija Fussi mjasiliamali kutoka Muheza Tanga.


Bi. Khadija Fussi mjasiliamali kutoka Muheza Tanga, anasema kuwa;

“…Nima uhakika kuwa Serikali imetusaidia kwa kiasi kikubwa maana awali wanawake ilikuwa huwezi kutoka nje na kufanya biashara zako lakini sasa tunatoka hadi nje ya nchi, Serikali imeweka usawa kwa jinsia zote ili nasi tuweze kufanya vizuri…kupitia hatua hiyo imetusaidia kwa kiasi fulani. Kwa utawala uliopita huduma za jamii zipo lakini kuna wajanja wachache ambao wanatubana hasa viongozi wa kati na chini.

Nashauri Serikali ijayo iendelee kutupa huduma kama hizi na fursa zaidi akinamama tunataka viongozi wa chini waache urasimu na kutuhudumia kulingana na maangizo ya viongozi wetu wa juu wa Serikali, maana viongozi wa juu wanatoa maelekezo mazuri lakini huku chini wanatunyanyasa.”

Bi. Catherine Mdaki kutoka Mkoa wa Tabora.

Bi. Catherine Mdaki kutoka Mkoa wa Tabora.


Bi. Catherine Mdaki kutoka Mkoa wa Tabora katika maoni yake anasema;

“Serikali iliyopita imetusaidia kwa kweli sisi tumepata mafunzo kuhusu ufungishaji na utafutaji masoko, kuna sehemu nyingi sasa tunapata mikopo nafuu ya kuweza kuendesha shughuli zetu. Mikopo ya masharti nafuu. Changamoto inayotugharimu ni usafirishaji wa bidhaa kwa wajasiliamali mfano sisi kutoka Tabora usafiri ni mgumu sasa unajikuta unaugawa mtaji wako kwa kusafirisha bidhaa.

Nashauri serikali ijayo ijitahidi kuwa karibu na kianmama kwa kuwa ndio waangalizi wa familia na tunamzigo mkubwa. Serikali iingie vijijini na kuwawezesha wanawake ili waweze kusonga mbele kimaendeleo,” alisema.

Mama Doricas wa Kilimanjaro

Mama Doricas wa Kilimanjaro


Mama Doricas wa Kilimanjaro anashauri kuwa;

“…Ukiniuliza Serikali kwa sisi wakinamama imetufanyia nini kukujibu moja kwa moja napata kigugumizi maana bado tuna changamoto kubwa sana…sisi wajasiliamali tunakumbana na changamoto kubwa, kwanza tukianzia vifungashio vya biashara zetu na namna ya kupata alama ya ubora wa bidhaa kiviwango inayotolewa na TBS, na TFDA bado kuna urasimu mkubwa sana sana.

Naukiangalia tunaingia kwenye soko la pamoja (EAC) naamini sisi kama wajasiliamali wa Tanzania tukiendelea hivi tutakuwa wasindikizaji kwe soko hilo maana hatuna nembo ya ubora inayoweza kukidhi soko la kimataifa. Nashauri kwa Serikali ijayo ije na Wizara ya Ujasiliamali inayojitegemea kwa jili ya kuinua uchumi wa taifa letu, na pia itusaidie kuna vikwazo vingine kwenye umiliki wa ardhi vinavyomfanya mwanamke asifikie malengo, kwetu mwanamke haruhusiwi kumiliki ardhi hata kama amenunua mwenyewe…Serikali ijayo itoe elimu zaidi kwa jamii yetu ili iweze kumuona mwanamke anahaki ya kumiliki ardha,” anasema.

Bi. Agnesta Lambikano

Bi. Agnesta Lambikano


Naye, Bi. Agnesta Lambikano, mjasiliamali kutoka Mkoa wa Kigoma anabainisha kuwa;

“…Serikali inayomaliza muda wake imetusaidia, imetuinua, imetusogeza angalau na kutujali mfano hivi tunavyoitwa kwenye maonesho kama haya, Maonesho ya 39 ya Biashara ya Kimataifa (sabasaba) tunaleta bidhaa zetu kutoka mikoa mbalimbali kama mafuta ya mawese, samaki, unga wa muhogo na dagaa hivyi inatufanya tuone nasisi Serikali inatujali.

Nashauri Serikali inayokuja ianzie hapa ilipoishia ya sasa na kutupeleka mbele zaidi sisi akinamama wajasiliamali ili tufikishe bidhaa zetu hata kimataifa, hasa kwa kututaftia masoko nje ya nchi,” anasema Bi. Lambikano.

Maoni hayo yalitolewa na baadhi ya Wanawake wajasiliamali walioshiriki Maonesho ya 39 ya Biashara Kimataifa (Sabasaba) katika Viwanja vya Mwalimu Julias Nyerere Barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam.
Itaendelea…