JK Atunukiwa Tuzo Nyingine

RAIS JAKAYA
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete ametunukiwa tuzo nyingine, zamu hii ikiwa imetolewa na wananchi wa Afrika Mashariki ambao wanaishi katika nje ya Afrika Mashariki na hasa Marekani (East African Diaspora) kutambua utawala bora wa uongozi wake katika nchi za Afrika Mashariki.
Tuzo hiyo imetolewa kwa niaba ya Wana-Afrika Mashariki hao na Baraza la Biashara la Wana-Afrika Mashariki Waishio Nje ya Afrika Mashariki – East African Diaspora Business Council (EADBC) ambalo linaunganisha wafanya biashara wa nchi za Afrika Mashariki wanaoishi nje ya eneo la Afrika Mashariki.
Tuzo hiyo kwa Rais Kikwete lilitolewa usiku wa Jumapili, Septemba 20, 2015, katika sherehe iliyofanyika katika Hoteli ya Hyatt Regency ya Dallas Kaskazini, Jimbo la Texas na kuhudhuriwa na Balozi wa Tanzania katika Marekani, Mheshimiwa Wilson Masilingi ambaye alipokea tuzo hiyo kwa niaba ya Rais Kikwete.
Awali, Rais Kikwete ambaye anaendelea na ziara yake ya kikazi katika Marekani alikuwa apokee tuzo hiyo mwenyewe lakini kwa sababu ya kutingwa na shughuli nyingi za kikazi katika miji ya New York na Washington, D.C alimwomba Balozi Masilingi kumwakilisha.
Rais Kikwete aliwasili nchini Marekani wiki iliyopita kuongoza vikao vya Jopo la Watu Mashuhuri Duniani ambalo limepewa jukumu la kupendekeza njia bora zaidi za jinsi dunia inavyoweza kukabiliana na magonjwa ya milipuko katika siku zijazo kufuatia balaa la ugonjwa wa Ebola ambao uliua zaidi ya watu 11,000 katika nchi za Guinea, Liberia na Sierra Leone katika muda mfupi.
Jopo hilo lenye wajumbe sita, wakiongozwa na Rais Kikwete, liliteuliwa Aprili mwaka huu na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Mheshimiwa Ban Ki Moon ambaye ametaka wana-jopo hao kuwasilisha ripoti yao kwake Desemba mwaka huu. Wajumbe wengine wanatoka Botswana, Brazil, Indonesia, Marekani na Uswisi.
Katika sherehe za usiku wa jana mjini Dallas, Balozi Masilingi alipokea tuzo hiyo ya utawala bora katika Afrika Mashariki kwa niaba ya Rais Kikwete kutoka kwa Mwenyekiti wa Baraza hilo Bwana David Mureeba, raia wa Uganda, ambaye amemweleza Rais Kikwete kuwa ni kiongozi wa mfano katika eneo la Afrika Mashariki na Bara zima la Afrika.
Tuzo hiyo ni ya tatu kutolewa kwa Rais Kikwete katika siku za karibuni. Taasisi ya East African Records karibu ilimtunukia Rais Kikwete tuzo kwa kutambua mchango wake katika kudumisha amani katika Tanzania na eneo zima la Afrika Mashariki. Rais Kikwete alipokea tuzo hiyo katika sherehe iliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam.
Kabla ya hapo, Rais Kikwete alitunukiwa tuzo ya uongozi bora iliyotolewa na Taasisi ya African Achievers Awards ya Afrika Kusini na kupokelewa kwa niaba ya Rais Kikwete na kupokelewa kwa niaba yake na Waziri wa Katiba na Sheria, Mheshimiwa Dkt. Asha Rose Migiro ambayo hatimaye alikabidhi tuzo hiyo kwa Rais Kikwete.
Rais Kikwete amewasili mjini Washington Jumatatu, Septemba 21, 2015, ambako kesho anatarajiwa kukutana na baadhi ya viongozi wa Serikali ya Marekani kujadiliana nao kuhusu masuala yanayohusu uhusiano kati ya Tanzania na Marekani.