WAPIGANAJI wa Libya wanasema hawataki kufanya majadiliano na Kanali Gaddafi, baada ya pendekezo hilo kutolewa na msemaji wa kanali. Na wapiganaji wa Libya piya wamesema wana wasiwasi juu ya usalama wa watu kama elfu 50, waliokamatwa na jeshi la Kanali Gaddafi katika miezi ya karibuni.
Wanafikiri watu hao wamezuwiliwa kwenye mahandaki mjini Tripoli, na wamewaomba watu wanaojua mahandaki hayo yaliko, wawape taarifa.
Piya wanasema shehena za mafuta na maji zinaanza kuwasili Tripoli leo, na meli zenye shehena za maji na mafuta ya vinu vya umeme, zinatarajiwa kutia nanga katika siku mbili tatu zijazo.
Kanali Gaddafi bado hajulikani aliko, lakini mtu anayefikiriwa kuwa msemaji wake, amelipigia simu shirika la habari New York, kusema Gaddafi yuko tayari kujadiliana na upinzani, ili kuunda serikali ya mpito.
Msemaji wa wapiganaji alieleza kuwa mto ambao ndio unaipatia Tripoli maji, umetiwa sumu na jeshi la Gaddafi, kwa hivo umefungwa. Katika ghala moja ya Tripoli, waandishi wa habari wamekuta maiti zilizoteketea za wanaume 50.
Inavoelekea waliuliwa na jeshi la Gaddafi, lilipokuwa likikimbia.
Shirika la habari la AP mjini New York, linasema limepigiwa simu na mtu waliyemtabua kuwa msemaji wa Kanli Gaddafi, Moussa Ibrahim, ambaye amejificha Libya.
Alisema kuwa Gaddafi sasa yuko tayari kujadili serikali ya mpito, na mazungumzo hayo yaongozwe na mwanawe, Saadi. Lakini kama Gaddafi mwenyewe hatosallim amri, pendekezo hilo litaonekana kuwa Gaddafi bado anjidanganya.