Kwanza tusameheane ndugu zangu kwa kupotea kidogo kwenye ukurasa huu kutokana na majukumu mengine ya maisha. Pia, napenda kuchukua nafasi hii kuwashukuru nyinyi wasomaji wa ukurasa huu wa “Chuo Cha Maisha”, ambao wengi wenu mmeandika email na kutufahamisha ni kiasi gani mmenufaika na makala hizi. Wengi mmetuma pongezi zenu na kusema kwamba mmejifunza mengi kutoka kwenye makala kama “Tabia Kuu Tano Za Watu Waliofanikiwa Kimaisha”, “Maamuzi Makuu Matatu Yanayoweza Kubadili Maisha Yako”, na nyinginezo. Hizi ni makala ambazo bado zinapatikana katika ukurasa huu.
Ndugu wasomaji, pamoja na kwamba tunashukuru na kufurahi pindi tupokeapo email zenu na kutufahamisha ni kiasi gani mmejifunza kupitia makala hizi, ingekuwa bora zaidi kama pia mngetumia japo dakika tano kuandika “comment” kwa faida ya wasomaji wengine pia. Kumbuka, huu ni ukurasa wa kuhamasishana katika suala zima la kuboresha maisha yetu. Hivyo basi, unapo shea ujumbe chanya kupitia comment ni watu wengi watasoma na kuhamasika kufanyia kazi kile walichokisoma, ambalo ndio lengo kuu haswa la Chuo Cha Maisha.
Baada ya muhtasari huo, ningependa kwenda moja kwa moja kwenye mada yetu ya leo kama kichwa cha habari kinavyosema “Je Unaishi Maisha Bora Au Bora Maisha?” Hili swali limenijia na kuamua kuliuza hapa baada ya kusoma kitabu cha aliyekuwa gwiji wa uhamisishaji jamii (Public Speaker) katika masuala ya kijamii na kiuchumi, marehemu Zig Ziglar (pichani juu), ambaye alikuwa ni Mmarekani na alifariki Mwezi wa 11, 2012 huko huko Marekani. Kitabu hicho kiitwacho “Over The Top” (kwa tafsiri ya neno kwa neno ni: “Juu ya kilele”, lakini maana iliyokusudiwa haswa ni “kilele” kwa maana kwamba ile hatua ya juu kabisa kimafanikio katika maisha) alikitoa mwaka 1997 (Revised Edition).
Katika kitabu hicho, kwa mujibu wa Ziglar, hatua ya juu kabisa kimafanikio katika maisha inategemeana na sifa 15 zifuatazo (Kutokana na nafasi, leo nitazitaja tano tu). Kwa maneno mengine, sifa hizi ndio zitakazo tusaidia kutambua kama tunaishi maisha bora au bora maisha?
Unaishi maisha bora (Over the Top), kama…….
1. Unatambua wazi wazi kwamba Kushindwa au kutofaulu ni matokeo tu, na sio mtu (yaani utu wako haubadiliki eti kwasababu umeshidwa kufanikisha au kufaulu suala fulani. Jipange upya halafu jaribu tena, kwani jana imeshapita na leo umejaaliwa siku mpya kabisa.
2. Hauna matatizo na yaliyopita (Past), Upo makini na kinachoendelea sasa (Present), na una matumaini tele na siku za usoni (optimistic about your future).
3. Unajua kwamba kushinda/mafanikio (a win) hakukujengi (kiutu) na kushindwa (a loss) hakukubomoi (kiutu). Hii ina undugu na namba moja hapo juu!
4. Umejaa imani (faith), matumaini, na upendo; na unaishi bila hasira, uchoyo, wivu, hatia (guilt), au mawazo ya kulipiza kisasi.
5. Umekomaa kiakili (au tuseme busara zimelala) kiasi cha kutotanguliza maslahi yako binafsi mbele, na umeweka msisitizo zaidi kwenye majukumu yako, badala ya haki zako.
Tukutane tena hapa, na tutaendelea kuhabarishana hizo sifa/ nguzo nyingine zilizobaki kutoka kwa mtaalam wetu Zig Ziglar.
Rungwe Jr.