Mama Salma ataka wanawake wajasiriamali wasaidiwe

Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA), Mama Salma Kikwete.

Na Anna Nkinda – Maelezo

WADAU wa maendeleo nchini wametakiwa kuwasaidia wanawake wajasiriamali kwa kuwapa fursa zilizopo ndani ya uwezo wao kwani wanawake hao huzalisha bidhaa za asili ya kitanzania ambazo hutumika ndani na nje ya nchi, na kwa kufanya hivyo huchangia kuongeza fursa za ajira na kuongeza pato la mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.

Wito huo umetolewa leo na Mke wa Rais, Mama Salma Kikwete wakati akizindua uchangishaji wa fedha kwa ajili ya kufanikisha maadhimisho ya Tamasha la Wanawake Wajasiriamali Tanzania kwa mwaka 2011 lijulikanalo kama Mwezi wa Wanawake Wajasiriamali (Month of Women Entrepreneurs – MOWE) katika Hoteli ya New Afrika jijini Dar es Salaam.

Zaidi ya shilingi milioni 55 pamoja na vifaa mbalimbali zilichangwa na wadau hao kwa ajili ya kufanikisha tamasha hilo ambalo linatarajia kufanyika Oktoba 30, hadi Novemba 4, mwaka huu katika viwanja wa Karimjee jijini Dar es Salaam.

Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) alisema kuwa kumuwezesha mwanamke kunasaidia jamii na taifa kupunguza umaskini wa kipato cha watu hivyo inachangia utekelezaji wa lengo la kwanza katika malengo ya millennia linalohusu kupunguza umaskini kwa nusu ifikapo mwaka 2015.

“Mimi binafsi nimeshiriki mara kadhaa katia shughuli za kuendeleza ujasiriamali kwa wanawake na nimejionea jinsi wanawake wakiwemo wenye ulemavu na waishio na Virusi Vya Ukimwi (VVU) wanavyotambua umuhimu wa kuongeza kasi katika juhudi za kuleta maendeleo kwao na kwa kila Mtanzania. Napenda kuwahakikishia kuwa jukwaa la MOWE ni mfano bora sana wa kuendeleza wanawake wajasiriamali”, alisema Mama Kikwete.

Mwenyekiti huyo wa WAMA pia aliwataka viongozi wa makampuni waliohudhuria katika hafla hiyo kupanga utaratibu wa kudumu wa kuchangia tamasha hilo ambalo Shirika la Kazi Duniani (ILO) limekuwa likisimamia kwa muda mrefu ili ILO itakapomaliza muda wake wa kusimamia tamasha hilo liendelee kufanyika.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa ILO nchini Alexio Musindo alisema kuwa wameshafadhili matamasha manne kama hayo na wataendelea kufadhili mengine kwani ukimuunga mkono mwanamke utakuwa umemuandalia maisha mazuri ya hapo baadaye pia wanawake wajasiriamali wamekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha kuwa wanapambana na umaskini na hivyo kuinua kipato cha familia zao.

Musindo alisema, “Moja ya malengo ya ILO ni kutoa nafsi kwa wanawake na wanaume ili waweze kufanya kazi kubwa, za kati na ndogo ambazo zitawaongezea kipato katika mazingira ya uhuru, usawa na ubinadamu kwani ujasiriamali ni chanzo kikubwa cha mapato, ajira na uzalishaji mali”.

Aliendelea kusema kuwa tamasha hilo litawakusanya maelfu ya wanawake wajasiriamali ambao wataweza kubadilishana mawazo, ujuzi pamoja na kujifunza teknolojia mbalimbali za kuzalisha bidhaa zao pia wataweza kupata masoko ya kuuza bidhaa zao na kujipatia fedha.

Naye Mwenyekiti wa kamati ya MOWE Elihaika Mrema alisema kuwa tukio hilo limekuwa likiadhimishwa hapa nchini tangu mwaka 2006 baada ya kujifunza kutoka nchi za Ethiopia mwaka 2004 na Zambia mwaka 2005.

Mrema alisema kuwa sababu za kuanzishwa kwa MOWE ni baada ya kutambua changamoto zilizokuwa zinawakabili wajasiriamali wanawake wakiwemo wenye ulemavu na waishio na VVU. Changamoto hizo ni uwezo mdogo wa kuyafikia masoko ya uhakika, ukosefu wa mitaji, maeneo bora ya kuzalishia bidhaa au kufanyia biashara, kushindwa kumudu gharama za utangazaji wa bidhaa au huduma wazalishazo na ugumu wa upatikanaji wa habari.

“Matokeo ya MOWE ni kutangaza kwa vitendo mafanikio ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii yaliyotokana na juhudi za wanawake wa rika zote, mijini na vijijini wakiwemo wenye ulemavu na waishio na VVU”, alisema Mrema.

Tamasha hilo ambalo hufanyika kila mwaka kwa mwaka huu linaratibiwa na Taasisi ya WAMA na litakusanya wadau kutoka mikoa yote nchini hasa wanawake wa rika zote wakiwemo wenye ulemavu na waishio na VVU huku kauli mbiu ikiwa ni “MIAKA 50 WANAWAKE WAJASIRIAMALI TUNAWEZA TUTUMIE FURSA”.