TCRA na Ufafanuzi wa Matangazo ya Moja kwa Moja…!

Makao Makuu ya TCRA ya Jijini Dar es Salaam

Makao Makuu ya TCRA ya Jijini Dar es Salaam

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
UFAFANUZI WA TANGAZO LILILOTOLEWA TAREHE 11 SEPTEMBA, 2015 KUHUSU VIPINDI VINAVYORUSHWA MOJA KWA MOJA WAKATI WA KAMPENI ZA UCHAGUZI MKUU

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) inapenda kutoa ufafanuzi kuhusu tangazo lake lililotolewa kwenye vyombo vya habari tarehe 11 Septemba, 2015 kuhusu vipindi vinavyorushwa moja kwa moja wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu. Ufafanuzi huu unatolewa kutokana na maoni mbalimbali ya wadau wakitaka ufafanuzi kuhusu tangazo hilo.
Mamlaka inatoa ufafanuzi kama ifuatayo:-
a) Kanuni za Huduma za Utangazaji (Maudhui) (Utangazaji wa Uchaguzi wa Vyama vya Siasa), 2015 ni Kanuni mbayo ipo kwa mujibu wa Sheria kama ilivyotolewa na Gazeti la Serikali la Tarehe 26 Juni, 2015. Kanuni hizi zinalenga kuweka utaratibu mzuri wa kutangaza shughuli za kampeni na
uchaguzi mkuu kuwa wa amani na utulivu;
b) Wadau wa sekta ya utangazaji walishirikishwa katika maandalizi ya Kanuni
hizi wakiwemo vituo vya utangazaji tarehe 28 Oktoba, 2014, Mitandao ya
kijamii tarehe 11 Novemba, 2014, Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na
Michezo tarehe 19 Desemba, 2014 na Tume ya Taifa ya Uchaguzi tarehe
14 Aprili, 2015;
c) Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania inasisitiza kuwa vyombo vinavyotoa huduma ya utangazaji vina wajibu wa kutoa taarifa kwa wananchi kuhusu uchaguzi bila ubaguzi ili wananchi wenyewe waelimike na hatimaye wafanye maamuzi sahihi kwa hiari yao kuchagua kiongozi anayefaa;
d) Mamlaka inafafanua na kusisitiza kuwa vyombo vya utangazaji
vinakumbushwa kuzingatia Kanuni za Huduma za Utangazaji
ISO 9001:2008 CERTIFIED
2
(Maudhui) (Utangazaji wa Uchaguzi wa Vyama vya Siasa), 2015,
hususani Kanuni zifuatazo;-
4. Kila mtoa huduma za maudhui atahakikisha kwamba:-
(f) haruhusu utangazaji wa jambo lolote linalohamakisha na
kuwagawa watu katika hali ya uchochezi;
(h) Utangazaji wa chaguzi unadhamiria kusisitiza ustahiki wa chaguzi
na kuhimiza ushiriki wa wananchi wote katika mchakato wa uchaguzi;
(i) wakati wa kipindi cha chaguzi habari zilenge juu ya masuala
muhimu na yenye maslahi kwa wananchi sio tu kutangaza matukio ya
vyama vya siasa au wagombea;
5. Kila mtoa huduma za maudhui atahakikisha kwamba vipindi na
uwasilishaji wake:-
(b) haujihusishi na kumkashifu au kumuumbua mgombea au mtu
mwingine yeyote au kauli mbaya juu ya uadilifu wa mtu;
(d) kipindi kisiwe na lugha ya kashfa, chuki au kufuru au lugha
yoyote (au toni ya lugha) inayoweza kuchochea vurugu au maasi;
(e ) kipindi kisiwe na kauli zinazoweza kumuudhi mtu yeyote kwa
sababu ya jinsia, jinsi, mbari, rangi, tabaka, imani au mahali pa asili.
(f) matangazo ya vyama vya siasa yatakuwa yale tu ambamo vyama
vinajitahidi kuelezea sera, mipango na malengo yake.

Hivyo basi, haikuwa lengo la taarifa hiyo kumzuia mtu yoyote kushiriki vipindi vya moja kwa moja (live Programmes) iwapo Kanuni zilizotajwa hapo juu zitafuatwa na kuzingatiwa.
Vituo vya utangazaji vinatakiwa kufuata kikamilifu Kanuni za Huduma za
Utangazaji (Maudhui) (Utangazaji wa Uchaguzi wa Vyama vya Siasa), 2015 na
kwamba vituo vya utangazaji vitawajibika na matokeo ya maudhui ya matangazo
ya moja kwa moja ambayo hayatozingatia Kanuni.
Mamlaka inatoa wito kwa vituo vya utangazaji kutumia weledi katika maamuzi ya
kihariri kuchanganua kipi kinafaa kutangazwa kwa maslahi ya Taifa.
IMETOLEWA NA:
MKURUGENZI MKUU MAMLAKA YA MAWASILIANO TANZANIA
TAREHE 13/09/2015