JULAI 21, 2011, Katibu Mkuu Kiongozi, Phillemon Luhanjo, akitumia madaraka yake ya Mamlaka ya Nidhamu ya Watumishi wa Umma, alitangaza hatua ya kumpa likizo ya malipo Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishatai na Madini, Bwana David Kitundu Jairo, ili kupisha uchunguzi aliokuwa ameuagiza ufanyike dhidi yake.
Bwana Luhanjo alichukua hatua ya kumsimamisha Bw. Jairo kufuatia tuhuma zilizokuwa zimeelekezwa dhidi yake na baadhi ya wabunge wakati wa mjadala kuhusu Makadirio na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka 2011/12 katika kikao cha Bunge kilichofanyika tarehe 18 Julai, 2011.
Katika mjadala huo, baadhi ya wabunge walihoji uhalali wa Wizara kuomba michango ya fedha kutoka kwenye Taasisi zilizoko chini ya usimamizi wake ili kusaidia Bajeti ya Wizara hiyo kupita kwa urahisi.
Kufuatia hatua hiyo ya kumsimamisha kazi Bw. Jairo, Katibu Mkuu Kiongozi alimwomba Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Bwana Ludovick Utouh kufanya ukaguzi maalum na uchunguzi wa awali juu ya tuhuma hizo.
Tarehe 9 Agosti, mwaka huu, 2011, Bw. Utouh aliwasilisha Ripoti yake kwa Katibu Mkuu Kiongozi, na tarehe 23, Agosti, 2011, Katibu Mkuu Kiongozi akiambatana na Bw. Utouh alitangaza mbele ya waandishi wa habari matokeo ya ukaguzi huo maalum na uchunguzi wa awali juu ya tuhuma dhidi ya Bw. Jairo.
Katika Ripoti yake mbele ya waandishi wa habari, Bw. Utouh alihitimisha: “Ukaguzi maalum haukuthibitisha kuwepo kwa usahihi wa tuhuma zilizotolewa dhidi ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini Bw. David Kitundu Jairo.”
Kufuatia Ripoti hiyo ya Bw. Utouh, Katibu Mkuu Kiongozi naye aliwaambia waandishi wa habari: “Matokeo ya uchunguzi huo ni kwamba tuhuma zilizotolewa Bungeni tarehe 18 Julai, 2011, hazikuweza kuthibitika. Kutokana na matokeo haya ya uchunguzi wa awali, mimi kama Mamlaka ya Nidhamu ya Katibu Mkuu, Nishati na Madini, Bwana David Kitundu Jairo, sitaweza kuendelea na hatua ya pili ya kumpa taarifa ya tuhuma (notice) na Hati ya Mashitaka kwa sababu Bwana David Kitundu Jairo, hajapatikana na kosa la kinidhamu (disciplinary offence) kwa mujibu wa Taarifa ya Ukaguzi Maalum.”
Alihitimisha: “Kufuatia matokeo ya taarifa hii ya awali na kwa mamlaka niliyonayo kwa mujibu wa Sheria Na. 8 ya Utumishi Umma ya Mwaka 2002 na kanuni zake za Mwaka 2003, NINAAMURU BWANA DAVID KITUNDU JAIRO AREJEE KAZINI KUANZIA SIKU YA JUMATANO, TAREHE 24 AGOSTI, 2011.”
KURUGENZI YA MAWASILIANO YA RAIS, IKULU, inapenda kutoa ufafanuzi kuwa baada ya kupokea taarifa ya uchunguzi ya CAG na uamuzi wa Katibu Mkuu Kiongozi kuhusu suala hilo asubuhi ya tarehe 25 Agosti, 2011, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, aliamua kuwa Ndugu Jairo asirudi kazini mpaka kwanza yeye Rais atapoamua namna gani ya kurudi kazini, lini na wapi.
Katibu Mkuu Kiongozi alifikisha uamuzi huo wa Rais kwa Ndugu David Jairo ambaye mapema asubuhi ya siku hiyo alikuwa ameripoti kazini. Ndugu Jairo alitii uamuzi huo wa Rais.
Tunapenda kusisitiza kuwa Mheshimiwa Rais hajawa kigeugeu kwa sababu alifanya uamuzi mmoja tu baada ya kupokea taarifa kutoka kwa Katibu Mkuu Kiongozi. Na uamuzi huo aliufanya kabla ya Bunge kulizungumzia suala hilo na hivyo uamuzi huo wa Rais haukutokana na shinikizo la Bunge. Pamoja na kumweleza Katibu Mkuu Kiongozi, Rais pia alimfahamisha Waziri Mkuu kuhusu uamuzi wake huo asubuhi hiyo ya tarehe 25, 2011.
Aidha, tunapenda kufafanua zaidi kwamba Katibu Mkuu Kiongozi ametimiza wajibu wake ipasavyo kama Mamlaka ya Nidhamu kwa Katibu Mkuu kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na Taratibu za Utumishi wa Umma. Mheshimiwa Rais, kwa upande wake, ametumia madaraka yake kama Mamlaka ya Ajira ya Katibu Mkuu. Hakuna suala la kujichanganya wala ukigeugeu ndani ya Serikali kuhusu suala hili.