Mifumo Biashara ya Nishati ya Jotoardhi Inatija

Baadhi ya wadau mbalimbali kutoka Kampuni ya Uendelezaji wa Nishati ya Jotoardhi Tanzania (TGDC), Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Wizara ya Nishati na Madini pamoja na TANESCO wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya warsha kuhusu Mifumo mbalimbali ya biashara kwa soko la Jotoardhi. Warsha iliyofanyika siku ya tarehe 2 – 4 Septemba, 2015 jijini Dar es Salaam.

Baadhi ya wadau mbalimbali kutoka Kampuni ya Uendelezaji wa Nishati ya Jotoardhi Tanzania (TGDC), Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Wizara ya Nishati na Madini pamoja na TANESCO wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya warsha kuhusu Mifumo mbalimbali ya biashara kwa soko la Jotoardhi. Warsha iliyofanyika siku ya tarehe 2 – 4 Septemba, 2015 jijini Dar es Salaam.

Na Benedict Liwenga-MAELEZO.

Mifumo ya kibiashara ya mvuke utokanao na nishati ya jotoardhi ina manufaa kwa Taifa kwani itasaidia kujenga uelewa kuhusu utaratibu unaoweza kutumika katika kupanga bei ikiwemo kudhibiti biashara ya jotoardhi ambapo kwa Tanzania, Taasisi inayohusika na udhibiti ni Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA).

Akiongea wakati wa kufunga Warsha ya siku mbili 2 Septemba – 4 Septemba, 2015 iliyofanyika jijini Dar es Salaam kwa kushirikiana na Shirika linaloshughulikia Nishati ya Jotoardhi Afrika Mashariki (EAGER) Meneja Mkuu wa Kampuni inayoshughulikia Nishati ya Jotoardhi Tanzania (TGDC), Mhandisi Boniface Njombe ameeleza kwamba, ili kuwa na uelewa mzuri kuhusu nishati hiyo hakuna budi kutambua aina gani ya biashara ya jotoardhi inayofaa kutumika hususani mfumo wa biashara ambapo kampuni ya Serikali inafanya kazi ya kufanya utafiti wa awali mpaka kuweza kubaini eneo la kuchimba mashimo ya kutolea mvuke chini ya ardhi, na pia ni pale ambapo Kampuni hiyo inaweza kuendeleza utafiti pamoja na kuchimba mashimo kadhaa na kuacha kazi nyingine za baadaye kufanywa na makampuni mengine ama wawekezaji kutoka nje.

Ameongeza kuwa hatua nyingine inayoweza kufanywa na Serikali ni pale Serikali yenyewe inaweza kuendeleza kuchimba mashimo kadhaa na kuendeleza zaidi kuchimba mashimo mengine mengi kwajili ya kutoa mvuke kwa ajili ya kuzalisha umeme.

“Hatua nyingine katika mfumo wa biashara hii ya jotoardhi ni pale ambapo Serikali kama Kampuni ya Umma inaweza kuendelea kuanzia kwenye utafiti hadi kwenye hatua ya kuzalisha umeme, lakini katika hatua hizi pia uko uwezekano katika ya Serikali na Kampuni binafsi kuweza kufanya kazi kwa pamoja, hivyo tunahitaji kuamua ni mfumo upi ambao tutautumia ili kuendeleza biashara hii ya jotoardhi”, alisema Njombe.

Akieleza kiini cha warsha hiyo, Mhandisi Njombe amesema kuwa lengo la warsha hiyo ni kuwa na uelewa mzuri kuhusu mifumo mizuri ya kibiashara ambayo itasaidia Tanzania na jamii kwa ujumla kunufaika na nishati hiyo lengo likiwa ni kupata faida kwa Serikali na kuweza kutumia faida hiyo kusaidia jamii ya Watanzania.

Naye Mhandisi kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Mhandisi Anastas Mbawala ameeleza kuwa wao ndiyo wadau wakubwa wa nishati kama hiyo kwani wanajukumu la kudhibiti nishati ya umeme na nyinginezo ikiwemo kupanga bei ambapo pia EWURA mwaka jana ilishaingia katika maandalizi ya mifumo ambayo itasaidia kudhibiti biashara ya umeme utokanao na jotoardhi ambapo jukumu walilopewa na Wizara husika lilikuwa ni kuandaa mikataba elekezi nao moja ya mikataba waliowahi kuiandaa ni ule unaohusiana na nishati ya jotoardhi.

“Ni wakati muafaka sasa kwa Wataalam kutoka nje kuipitia mikataba yetu elekezi ili waweze kujiridhisha nayo na kama kuna maoni yoyote waweze kutoa ili pindi tunapoanza kuitumia iwe tayari imeshaboreshwa”, alisema Mbawala.

Aliongeza kuwa katika masuala ya udhibiti kitu kikubwa kinachoangaliwa ni Sheria, Taratibu na Kanuni ambapo EWURA kazi yao kubwa ni kudhibiti nishati na maji na sio kudhibiti maji ya kwenye mabwawa, bali inadhibiti maji yanayouzwa kwa watu.

“EWURA imeweza kudhibiti gesi asilia kwa kutumia mikataba na sera na Sheria zilizokuwa za mafuta lakini mwaka huu imekuja Sheria mahususi inayozungumzia masuala ya petroli na gesi, pia kwa upande wa Sheria ya Maji nayo iliboreshwa ambapo inamuona mdhibiti, hivyo nishati hii ya jotoardhi tunaamini itasaidia kupunguza gharama za umeme sisi wadau wote tunahaja ya kushirikiana kwa pamoja na kuonyesha mahusiano katika masuala haya muhimu”, aliongeza Mbawala.