Na Janeth Mushi, Arusha
WAKILI wa Serikali, Edwin Kakolaki ameiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Arusha kutoa onyo kali katika kesi inayowakabili viongozi wa juu wa CHADEMA, hasa kwa washtakiwa wawili yaani mchumba wa Dk. Wilbroad Slaa, Josephine Mshumbuzi na Dadi Igogo kwa kile kutohudhuria mahakamani huku wakiwa na sababu zisizo na msingi.
Kakolaki aliomba mahakama kupanga tarehe ya usikilizwaji wa
awali wa kesi hiyo kwani baadhi ya washtakiwa katika shauri hilo
wamekuwa wakitoa sababu zisizokuwa na msingi kukwamisha usikilizwaji, huku akitolea mfano sababu ya kusafiri kwa mbunge wa Moshi Mjini, Philemon Ndesamburo kwenda Uingereza kwa uchunguzi wa afya na Marekani kwa ajili ya shughuli za Manispaa kama barua iliyotoka kwa Spika wa Tanzania Anna Makinda inavyoonesha.
Mbele ya Hakimu mkazi wa mahakama hiyo, Charles Magesa Wakili huyo wa Serikali aliomba mahakama kutoa onyo kwa mshtakiwa Derick Magoma anayedaiwa kwenda Igunga na wakati akirudi gari lake kuharibika njiani katikati ya Babati na Igunga huku akijua anahitajika mahakamani hapo.
Alidai kuwa Josephine awali ilitolewa taarifa mahakamani hapo kuwa hataweza kuhudhuria kesi mpaka atakapojifungua lakini pia alikuwa anaendesha gari na kuibiwa baadhi ya vitu huko Dar es Salaam wakati mahakamani ilielezwa kuwa anatakiwa kupumzika kutokana na matatizo ya ujauzito hivyo anatakiwa kuhudhuria mahakamani hapo bila kukosa kwani kuna washtakiwa wenzake wapo mahabusu na wana watoto lakini siku ya kesi wanahudhuria mahakamani hivyo na yeye ni lazima ahudhurie.
Wakili upande wa Utetezi, Method Kimomogolo alidai ni halali kwa Josephine kuendelea kupumzika kwa siku 84 kutokana na uzazi lakini kama wakili Kakolaki anataka aje mahakamani hapo na mtoto kama kielelezo aseme lakini kisheria bado ni mzazi na anahitaji kupumzika.
Kimomogolo alidai kuwa inawezekana wakili Kakolaki anataka Josephine aje na mtoto kama kielelezo toka alipojifungua ni mwezi mmoja sasa hivyo unajua kabisa mzazi anatakiwa kupumzika kwa miezi mitatu awe ameajiriwa au hajaajiriwa hivyo aliiomba mahakama isitoe onyo kwani sababu zake ni za msingi pia kuhusu Igogo kutohudhuria mahakamani ni kutokana na kuumwa akiwa Kigoma na alishindwa kutoma faksi za kudhibitisha hilo kutokana na umeme kukatika .
“Hivi unataka mtoto aje mahakamani kama kielelezo au unatakaje pia suala la Igogo ni tatizo la umeme na wewe kwa kuwa ni wakili wa Serikali utueleze sababu za umeme kutokuwepo mahakamani hapa pia nakuomba hakimu usitoe onyo kwa washtakiwa hao na mshtakiwa Igogo atakapokuja atatoa taarifa za kuumwa kwake, Magoma naye ametoa
sababu hivyo hakuna sababu ya onyo”.
Baada ya mabishano hayo ya kisheria, Hakimu Charles Magesa alisema
amekubaliana na ombi la wakili Kimomogolo la kutotoa onyo na kutoa
wito kwa wakili huyo kuhakikisha siku ya kesi itakapotajwa tena lazima mshtakiwa Josephine ahudhurie mahakamani hapo na washtakiwa wengine ili ianze kusikilizwa.
Magesa alimtaka mshtakiwa Igogo ahudhurie mahakamani hapo akiwa na nakala ya udhibitisho kama kweli alikuwa anaumwa na kumtaka Magoma kuhudhuria siku ya kesi kama inavyotakiwa.
Akizungumzia suala la Ndesamburo kwenda kwenye matibabu, magesa alisema tatizo limeanzia kwenye barua ya ruhusa iliyotolewa na Spika wa Bunge, Anna Makinda dhidi ya Ndesamburo kwani haijaonesha tarehe ya kurudi nchini lakini aliongeza kuwa kama Septemba 23 kesi itakapokuja kwa usikilizwaji wa awali atakuwa hajarudi basi sheria itaangalia ili kesi hiyo isikilizwe. Kesi hiyo imeahirishwa hadi hapo Septemba 23 mwaka huu wka ajili ya
usikilizwaji wa awali.