MISA Yaendesha Mafunzo kwa Wanahabari Dar

WANAHABARI WAKIWA KAZINI

Na Geofrey Mushi. Dar es salaam.

Taasisi ya vyombo vya Habari kusini mwa Afrika (MISA) yenye Makao yake Makuu nchini Namibia imeendesha Mafunzo ya siku moja kwa Wanahabari Dar es Salaam katika Hoteli ya Kebby’s ambapo Mtaalamu wa Maswala ya Habari kutoka MISA, Gasirigwa GS alisisitiza juu ya Waandishi wa Habari kuzingatia Misingi na Maadili ya Habari kwa ujumla ili kutoburuzwa na Wanasisa hasa katika kipindi kama hichi cha Uchaguzi.

Mwanasheria na Mwanahabari James Marenga amewaasa Wanahabari juu ya Changamoto mbalimbali hasa kwenye Sheria zilizopo kushindwa kukidhi Matakwa ya Ibara ya 18 ya Katiba ambayo inatoa Haki kwa mtu yeyote kutafuta na kusambaza Habari bila kuathiri Masharti ya Sheria za Nchi.

Katika Mafunzo hayo, James Marenga aliwasii Wanahabari kuhakikisha wanashiriki kwenye kila Harakati za kuboresha Tasnia nzima ya Habari hasa kwenye upande wa Sheria mbalimbali za Habari, katika upande wa Sheria alieleza juu ya baadhi ya Miswada ambayo imewahi kupelekwa Bungeni kubana Uhuru wa Habari na hata kutishia kuivuruga Tasnia nzima ya Habari.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Jamii Media, Maxence Melo akizungumza kwa upande wake alionya juu ya kukosekana nia ya dhati hasa kwa Watawala kuboresha Uhuru wa Habari hapa nchini, na akizungumzia Sheria mpya ya Makosa ya Mtandaoni (Cyber crime) haijatungwa kwasababu ya Uchaguzi bali misukumo toka kwa Wahisani na hivyo si rahisi kujibu Changamoto zetu binafsi kama Taifa.

Kwa upande wa Wanahabari waliofika kwenye Mafunzo hayo waliainisha Changamoto mbalimbali hasa kwenye Mfumo wa Umiliki wa Vyombo vya Habari katika Nchi yetu kuwa chini ya Wanasiasa, Wafanyabiashara, Mashirika, Serikali, na hata Wanahabari wenyewe, hivyo kuleta Mkanganyiko kwenye Tasnia ya Habari kwa kuwa baadhi ya Vyombo kuendeshwa kwa Maslahi binafsi.