Sumaye Ang’oka CCM, Ajiunga na UKAWA

Waziri Mkuu mstaafu, Fredreck Sumaye (kushoto), akizungumza na wanahabari wakati akitangaza kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), leo mchana.

Waziri Mkuu mstaafu, Fredreck Sumaye (kushoto), akizungumza na wanahabari wakati akitangaza kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), leo mchana.

 Waziri Mkuu mstaafu, Fredreck Sumaye (kulia), akipeana mkono na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe Dar es Salaam leo mchana, baada ya kujiunga na chama hicho. Anayeshuhudia katikati ni Mgombea urais wa Tanzania kupitia chama hicho, Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa.
 Sumaye akisisitiza jambo
Sumaye (wa tatu kulia), akiwa na viongozi wanaunda Umoja wa Katiba (UKAWA) baada ya kuondoka CCM na kujiunga na Chadema.
Na Joachim Mushi, Dar es SalaamHATIMAYE aliyekuwa Waziri Mkuu mstaafu Fredrick Sumaye amekihama rasmi Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kuamia vyama vinavyounda ushirikiano wa UKAWA akidai ameenda upande huo kuongeza nguvu kuelekea kushinda uchaguzi mkuu kwa upande wa upinzani.

Sumaye ameng’oka rasmi CCM leo alipozungumza na vyombo vya habari jijini Dar es Salaam ndani ya Hoteli ya Bahari Beach huku akisisitiza hajakiama chama hicho kwa kwa kile kumchukia mgombea wa chama hicho, Dk. John Magufuli bali kutokana na kutoridhishwa na mwenendo wa chama hicho.

Alidai CCM haijuti na wala kusikitika kuhama kwake kwani yeye hakuwa na majukumu yoyote ndani ya chama hicho ila ameamua kuingia upinzani ili kuunga mkono mabadiliko ambayo wananchi wanayataka na kuongeza nguvu waweze kushinda uchaguzi mkuu.

Hata hivyo hakutaja chama ambacho amejiunga nacho kati ya vyama vinavyounda umoja huo yaani Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi pamoja na NLD, lakini alisema amejiunga na UKAWA na chama atakachojiunga kitajulikana mbele.

Alisema yeye kutoka CCM haina maana kwamba anakidhohofisha chama hicho bali anakijenga ili kupambana kwa nguvu na upinzani mkali kutoka UKAWA. “…Napenda kuwahakikishia kutoka kwangu CCM hakukidhohofishi chama hicho bali anakiimarisha zaidi kwani kwa sasa watapambana na upinzani mkali jambo ambalo ni kukiimarisha chama hicho…kwasababu sasa upinzani utakuwa mkali,” alisema Sumaye.

Akifafanua zaidi alisema kujiunga na UKAWA hakuna maana kuwa ana maslahi yoyote binafsi wala kudai cheo, nafasi yoyote lakini yupo tayari kusaidia kupiga kampeni ili upande wa upinzani uwe na nguvu kuelekea kampeni za uchaguzi.

“…Sijaingia huku sijui kwasababu Lowassa anatoka Kaskazini kama watu wengine ambao sijui wana akili za wapi waliwahi kusema kiongozi wa nchi hii hawezi kutoka Kaskazini…sijui Kaskazini wanatoka mafisi, lakini mimi sijaja huku kwasababu anatoka Kaskazini hata kidogo na mimi siasa ya ukanda nilisha ipiga vita sana, siasa ya udini nilisha ipiga vita sana, imetokea wengi waliopo UKAWA watatoka Kaskazini na mimi nataka kuimarisha upinzania,” alisema.

Alisema anaamini upande wa UKAWA utashinda kwa kiasi kikubwa katika uchaguzi huu na hautakuwa na kazi kuendesha Serikali kwa kuwa Edward Lowassa ni mzoefu serikalini na ameshika nafasi mbalimbali ndani ya Serikali hivyo hata kuwa na ugumu wa kuongoza Serikali hiyo.

“…Watu wanashangaa mimi kwenda UKAWA sinataka kwenda kuimarisha upande huo ili kuchochea maendeleo na nchi iende vizuri…hilo ndio lengo langu la kwenda UKAWA, kwasababu tunaona CCM imezubaa wanajigamba tu watashinda wananchi wamekwisha choka wanataka mabadiliko…,” alisema Fredrick Sumaye na kuwataka wanachama wenye nia nzuri CCM waingie UKAWA ili kuweza kuiletea nchi maendeleo.

Kiongozi huyo hivi karibuni mitandao ya kijamii iliripoti kwamba ametangaza kukihama chama cha mapinduzi lakini hakukanusha wala kukubali juu ya taarifa hizo hadi leo anakuja kuibuka na kutangaza rasmi kukihama chama hicho. Kiongozi huyo anang’oka CCM huku ikijiandaa kuzinduwa kampeni zake rasmi kesho jijini Dar es Salaam katika viwanja vya Jangwani.