MSAJILI wa vyama vya siasa nchini ameonya tabia ya baadhi ya wanachama na mashabiki wa baadhi ya vyama ambao wameibua mtindo wa kuwazomea wanachama wa vyama vingine na wakati mwingine kuwarushia mawe wanachama hao wanapokuwa wamevaa rangi ya vyama vyao.
Jaji Francis Mutungi ametoa onyo hilo katika taarifa yake aliyoitoa kwa vyombo vya habari jana akiwataka viongozi wa vyama kuwa makini katika kipindi hiki cha uchaguzi na pia kuwazuia wanachama na mashabiki wao kutotenda kinyume na sheria za nchi.
Amesema tabia ya zomea zomea hiyo sio zuri na inaweza kusababisha vurugu na hatimaye uvunjifu wa amani jambo ambalo ni kinyume na sheria. “…Siku za hivi karibuni kumejitokeza tabia ya baadhi ya wanachama na mashabiki ya baadhi ya vyama kuwazomea na hata kuwarushia mawe wanachama na mashabiki wa vyama vingine hasa pale wanapovaa sare za vyama vyao,” alisema Jaji Mutungi katika taarifa hiyo.
Alisema amewataka viongozi wa vyama vyote kutoa maelekezo kwa wanachama na mashabiki wao kuacha tabia kama hizo kwani kipindi chote cha uchaguzi kinahitaji utulivu na uvumilivu wa kisiasa, huku akiwataka kufanya kampeni za kistarabu ambazo haziwezi kuchochea vitendo vya uvunjifu wa amani.
Aidha alisema vyama vyote vinawajibu wa kisheria na kijamii kudhibiti vitendo vyote vya wanachama wao ambavyo vinaweza kusababisha uvunjifu wa amani.