Na Mwandishi Wetu, Tanga
WAJASIRIAMALI mkoani Tanga wametakiwa kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Mradi wa Muunganisho Ujasiriamali Vijijini (MUVI) ili kufanikisha lengo la kuunganisha nguvu za wajasiriamali na hatimae kujikwamua na umasikini.
Rai hiyo imetolewa hivi karibuni na Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Tanga, Ndibalema Kisheru katika uzinduzi wa shughuli za wadau wa habari wa mradi wa MUVI mkoani hapa.
“Tunafahamu kuwa lengo kuu la Mradi wa MUVI ni kukuza na kuimarisha biashara za Wajasiriamali hasa wale wa vijijini ambao kwa sehemu kubwa shughuli zao zimejikita katika kutegemea mazao ya alizeti, machungwa na maembe katika mkoa wetu, hivyo nawaomba ndugu zangu tusiupuuze mradi huu,” alisema Kisheru.
Alisema MUVI inawajengea uwezo wajariamali kwa njia mbalimbali zikiwemo kuwaunganisha katika vikundi ili waweze kutambuliwa na wadau wengine wenye malengo yanayoshabihiana. Na pia kukusanya nguvu za pamoja ili kumudu huduma na rasilimali ambazo zingetafutwa na mtu mmoja mmoja ingekuwa vigumu ama gharama kubwa.
Aidha Kisheru aliongeza kuwa kuwa kila mmoja anafahamu kwamba kwa kuwa katika vikundi wajasiriamali wanakuwa na sauti inayoweza kusikika katika ushawishi na utetezi na kupitia vikundi wanaweza kuimarisha mawasiliano na wadau nje ya vikundi ikiwemo Serikali kuanzia kijijini mpaka ngazi ya taifa.
Alisema kupitia wadau wa habari ni dhahiri kuwa sauti za kundi hilo zitasikika zaidi na kuzidi kufanikiwa katika shughuli zao.
Mradi wa MUVI ulitambua umuhimu wa kuwaunganisha wajasiriamali katika ngazi mbalimbali zikiwemo za Wilaya, Mkoa na hata Taifa hivyo ikaweka bayana nia ya kuwa na vyombo vinavyowaunganisha wajasiriamali wote katika milolongo ya thamani iliyo katika Mradi.
Naye Mkurugenzi wa Habari wa Mradi wa MUVI Tanzania, Joseph Makanza amesema mradi wa MUVI unafanya kila liwezekanalo katika kuhakikisha taarifa zinawafikia wajasiriamali vijijini, kwani wamekwisha anza kutumia njia mbalimbali za mawasiliano zikiwemo radio, ujumbe mfupi wa maneno kwa simu (sms) na mbao za matangazo.
“Tunahakikisha upatikanaji wa pembejeo za kilimo, kuibua na kutekeleza ubunifu katika nyanja za masoko, teknolojia na sera ili kuinua ufanisi katika milolongo ya thamani ya mazao ya alizeti, machungwa na maembe,” alisema Makanza
Hata hivyo mradi unawaunganisha wajasiliamali katika vyama, kuunda majukwaa, kuwajengea uwezo ili waweze kukopeshwa na taasisi za fedha na kuweza kumudu huduma za uwezeshaji zinazotolewa na soko la huduma. Mradi wa MUVI Tanzania ulianzishwa na Serikali ya Tanzania na unasimamiwa Shirika La Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO).