Mbowe Alazwa Muhimbili, Azungumza na Waandishi Hospitalini

Freeman Mbowe akizungumza na waandishi wa habari Muhimbili leo. Kulia ni Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi James Mbatia akiwa naye.

Freeman Mbowe akizungumza na waandishi wa habari Muhimbili leo. Kulia ni Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi James Mbatia akiwa naye.

Na Mwandishi Wetu

MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe amelazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, kitengo cha moyo baada ya kuugua gafla akiwa kwenye msafara wa mgombea wa urais kupitia Chama hicho, Edward Lowassa na kukimbizwa hospitalini.

Akizungumza na waandishi wa habari leo akiwa Hospitali ya Muhimbili ya jijini Dar es Salaam Mbowe alisema anaendelea vizuri na matibabu na anaweza kuruhusiwa baada ya saa 48. Alisema baada ya uchunguzi madaktari wamemwambia anaonekana alifanya kazi mfululizo bila kupata nafasi ya kupumzika jambo ambalo limemletea uchovu (fatique) wa mwili hivyo hali yake kubadilika akiwa kwenye msafara.

Mbowe alikuwepo jana kwenye msafara wa Lowassa akiwa na viongozi wengine wa Chadema ambapo walikuwa wamekaa juu ya magari na kuwapungia mikono wananchi na wanachama waliojitokeza kumsindikiza mgombea wa chama hicho pamoja na mgombea mwenza kwenda kuchukua fomu ya kuomba kuteuliwa kugombea nafasi ya urais wa Tanzania katika ofisi za Tume ya Taifa ya Uchaguzi.

Akiwa njiani kuelekea viwanja vya Biafra Kinondoni hali yake ilibadilika ghafla hivyo kulazimika kukimbizwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa matibabu zaidi, aliongozana na baadhi ya viongozi aliokuwa nao gari moja pamoja na walinzi wake.

Taarifa zilizagaa kwenye mitandao ya kijamii kuwa Mbowe ameanguka gafla jambo ambalo alilipinga akizungumza na waandishi wa habari; huku akisisitiza alijisikia vibaya hivyo kuteremka juu ya gari na kukaa ndani ya gari kabla ya viongozi wenzake kuanza kumpa huduma ya kwanza huku wakielekea hospitalini.

Aidha kiongozi huyo amewataka Watanzania na wanachama wa Chadema kutokuwa na hofu kwani anaendelea vizuri na matibabu na baada ya hapo atarejea kazini kama kawaida.