UMOJA wa Ulaya umesema uko tayari kupeleka msaada wa matibabu nchini Libya. Utapeleka mahitaji yanayotakika kwa dharura katika hospitali nchini humo, kuwasaidia raia wengi waliojeruhiwa katika vita. Shirika la misaada la Medicins Sans Frontiers limesema hali katika hospitali za mji mkuu Tripoli inakaribia kuwa balaa, kwa kuwa mahitaji yamepungua mno wakati wa mapigano ya miezi sita.
Kamishna wa Umoja wa Ulaya anayehusika na kuratibu juhudi za kukabiliana na mizozo, Kristalina Georgieva, ametenga euro milioni 80 kwa ajili ya mzozo wa Libya, zikiwemo euro milioni 10 kwa msaada mara tu mji wa Tripoli na miji mingine ya pwani itakapofunguliwa kuruhusu misaada ya kibinadamu. Kamishna huyo amesema misaada imeshapelekwa katika maeneo ya Libya yanayoweza kufikika na kwamba washirika wa Umoja wa Ulaya wataweza kuanza kazi mara tu mapigano yatakapomalizika.
-BBC