Na Mwandishi Wetu, Arusha
ALIYEKUWA Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Halmshauri ya Wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha, Elias Ngorisa na Katibu wa Fedha na Uchumi wa CCM Wilaya ya Ngorongoro, Arusha, Kaigil Ngukwu ambaye pia alikuwa ni Diwani wa CCM Kata ya Enguserosambo, wamehama chama hicho na kuhamia Chadema.
Wakizungumza kwa pamoja na waandishi wa habari jana katika Ofisi za Chadema Mkoa wa Arusha, viongozi hao walisema kuwa wamelazimika kuhama CCM kutokana na ukiukwaji wa kanuni na katiba uliofanywa na viongozi pamoja na kutaka mabadiliko ambayo wameyakosa ndani ya CCM.
Ngorisa ambao pia walikuwa wameambatana na viongozi wa kimila Malaigwanani wakiongozwa na Laigwanani Laurance Ngorisa walipokelewa na Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari.
Wakizungumza mara baada ya kukabidhiwa kadi Ngorisa alisema, amefikia uamuzi huo baada ya kubaini mifumo iliyopo ndani ya CCM imekuwa ikinyima haki kwa wanachama wake. Alisema ameamua kuondoka CCM kwani kumekuwa na ukiukwaji mkubwa wa kanuni ndani ya chama hicho pamoja na vitendo vya rushwa hasa wakati wa uchaguzi.
Walisema kuwa hivi karibuni wanatarajia kupokea viongozi na wanachama wa CCM kutoka wilayani humo na kuwa kwa pamoja wanamuunga mkono mgombea Urais wa UKAWA, Edward Lowassa, aliyechaguliwa hivi karibuni.