RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete, Agosti 4, 2015, ametia saini Miswada ya Sheria mitano hadharani ikiwa ni hatua yake ya mwisho kabisa kuridhia Miswada ya Sheria akiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Katika sherehe iliyofanyika katika Ukumbi mpya wa Ikulu, Dar Es Salaam, Rais Kikwete ameridhia Muswada wa Sheria ya Mafuta na Gesiasilia, Muswada wa Uwazi na Uwajibikaji, Muswada wa Usimamizi wa Mapato ya Mafuta na Gesiasilia, Muswada wa Masoko ya Bidhaa na Muswada wa Tume ya Walimu.
Katika sherehe hizo zilizohudhuriwa na mamia ya wageni waalikwa, mawaziri wanaohusika na sekta hizo, George Simbachawene ambaye ni Waziri wa Nishati na Madini, Saada Mkuya ambaye ni Waziri wa Fedha na Dk. Shukuru Kawambwa ambaye ni Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi wametoa maelezo ya miswada hiyo mitano kabla haijaridhiwa na Rais Kikwete.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Mohamed Gharib Bilal na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue pia wamehudhuria sherehe hizo ambazo vile vile zimehudhuriwa na mawaziri wa Serikali, mabalozi, wawakilishi wa taasisi zisizokuwa za Kiserikali (NGO’s) na wadau wengine wa sekta ambazo Miswada yake imeridhiwa.
Hiyo ni mara ya pili kwa Rais Kikwete kuridhia Miswada ya Sheria hadharani. Mara ya kwanza ilikuwa mwaka 2009 wakati Rais Kikwete aliporidhia hadharani Muswada wa Sheria ya Matumizi ya Fedha katika Uchaguzi.
Aidha, hiio ni mara ya mwisho kwa Rais Kikwete kuridhia Miswada ya Sheria nchini kabla ya kuondoka madarakani mwanzoni mwa Novemba, 2015. Rais tayari amelivunja Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.