WAZIRI Mkuu mstaafu na mwanachama mpya wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Edward Lowassa leo amechukua fomu za kugombea nafasi ya urais kupitia chama hicho. Lowassa ambaye msafara wake ulikuwa na wananchi wengi kiasi ambacho uliwashinda vijana wa ulinzi wa CHADEMA, aliwasili katika Makao Makuu ya chama hicho majira ya saa sita na nusu na kupokelewa na wanachama wengi waliokuwa wamejipanga pembeni mwa barabara ya mtaa zilizopo ofisi za chama hicho.
Akizungumza kabla ya mgombea huyo kukabidhiwa fomu, Mwanasheria Mkuu wa Chama hicho, Tundu Lissu(Mb) alisema katiba ya Chadema na ile ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inamruhusu Lowassa kugombea urais endapo atapitishwa na chama hicho. Alisema Lowassa anaruhusiwa kuzunguka ili kujitambulisha kwa wananchi kwamba ameomba kugombea nafasi hiyo na wamuunge mkono.
Lissu alisema taarifa zinazotolewa kuwa chama hicho kimegawanyika baada ya kuingia Lowassa ni za uzushi na kuwataka WanaChadema na wananchi wazipuuze, kwani hakuna ukweli wowote wa suala hilo. Aliwataka viongozi wa Chadema pamoja na Lowassa kujipana ili kuhakikisha wanashinda viti vingi vya nafasi ya ubunge na cha urais ili waweze kuunda Serikali. Alisema wanatakiwa kushinda zaidi ya viti vya ubunge 133 ili kupata sifa kikatiba ya kuunda Serikali.
“…kazi iliyopo mbele yetu ni kuhakikisha tunashinda uchaguzi wa rais na tunashinda viti vingi zaidi ili tuweze kuunda Serikali ijayo ya awamu ya tano itakayokuwa ya kwanza isiyo ya CCM. Mheshimiwa Lowassa kuanzia leo tutakapo kupa fomu hizi una haki ya kuzunguka Tanzania nzima na kuzungumza na Watanzania kuwaambia kuwa wewe ni mgombea uliyependekezwa na Chadema kugombea nafasi hiyo,” alisema Lissu.
Baada ya Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kumkabidhi fomu Lowassa walijitokeza baadhi ya wanachama na kumchangia fedha za kulipia fomu hiyo na kumkabidhi ili aongezee na kulipia fomu aliyochukua. Kwa upande wake Lowassa akizungumza mara baada ya kuchukua fomu aliwashukuru wanachadema kwa kumchangishia fedha za kulipia fomu na kudai hana cha kuwalipa lakini washirikiane aweze kushinda uchaguzi huo na matunda yake watayaona.
Alisema watu wanaoendelea kumshambulia mara baada ya kujiunga na Chadema wanapoteza muda bure kwani hawezi kurudi nyuma. Wale wachambuzi wa mambo wanaonishambulia baada ya kujiunga Chadema wanapoteza muda mimi sitarudi nyuma…mimi ningependa kuwaambia natekeleza maelekeza wa Baba wa taifa Mwalimu Julias Nyerere alisema ‘Watanzania wanataka mabadiliko wasipoyapata ndani ya CCM watayatafuta nje ya CCM, mimi nimeridhika ndani ya CCM mabadiliko hayo hayawezi kupatikana, lakini Watanzania wanataka mabadiliko mabadiliko haya watayapata kwa kura zetu…wanaotaka mabadiliko ni wengi tukijipanga vizuri tutashinda uchaguzi,” alisema Lowassa.
Kwa upande wake Mbowe alisema Agosti 4, 2015 Chadema itakuwa na Mkutano Mkuu ambao kwa kushirikiana na vyama vinavyounda UKAWA watapitisha jina la mgombea Urais pamoja na mgombea mwenza na pia kupitisha ilani ya uchaguzi ambayo imeridhiwa na vyama vyote vinavyounda umoja wa UKAWA kabla ya kuanza mchakato wa kampeni.
Alisema bado wanakipindi kikumu cha majadiliano na maridhiano ya vyama vyote vinavyounda UKAWA hivyo kuwataka wananchi wawaombee ili waweze kupita salama katika kipindi hicho kigumu. Kuanzia Agosti 5 hadi 7, 2015 Kamati Kuu itapitisha wagombea wa Ubunge kwa utaratibu ambao pia utatumiwa na vyama vyote vinavyoshirikiana katika umoja wa UKAWA.