Dk shein amzika Mbunge Silima

Waombolezaji

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein leo ameongoza mazishi ya marehemu Mhe. Mussa Khamis Silima, Mwakilishi wa Jimbo la Uzini na Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano Tanzania.

Katika mazishi hayo yaliyofanyika kijini kwao marehemu huko Kiboje Mwembeshauri Wilaya ya Kati, Mkoa wa Kusini Unguja viongozi mbali mbali walihudhuria akiwemo Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania Mhe. Mohamed Kharib Bilal.

Viongozi wengine waliohudhuria ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, Spika wa Baraza la Wawakilishi Mhe. Pandu Ameir Kificho, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Anna Makinda, Waziri Mkuu Mstaafu Edward Lowasa, Wabunge, Wawakilishi, Mawaziri wa Serikali zote mbili pamoja na viongozi wa vyama vya siasa na viongozi wengine na mamia ya wananchi.

Mara baada ya mazishi hayo yaliyofanyika saa saba za mchana huko Kiboje Mwembeshauri, viongozi mbali mbali waliwakilisha salamu zao za pole kwa ndugu na wanafamilia pamoja na kutoa ubani kwa wafiwa.

Miongoni mwa viongozi waliotoa salamu hizo ni pamoja na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Mhe. Vuai Ali Vuai ambaye alitoa salamu kwa niaba ya Chama Cha Mapinduzi, na viongozi wake wote akiwemo Mwenyekiti wa Chama hicho Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete. Mhe. Pandu Ameir Kificho alitoa salamu za pole kwa niaba ya Baraza la Wawakilishi.

Wengine ni mwakilishi wa Wabunge wa Zanzibar Mhe. Hamad Rashid,Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni Mhe. Mboe, Mhe. Simba Chaweni ambaye alitoa salamu za pole kwa niaba ya Bunge la Jamhuri ya Muungano.

Aidha, Mhe. Willium Lukuvi alitoa salamu za pole kwa niaba ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mhe. Mohamed Aboud alitoa salamu za pole kwa niaba ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Nao wanafafamilia walitoa shukurani kwa viongozi wote waliohudhuria katika mazishi hayo pamoja na kutoa shukurani kwa msaada mkubwa walioupata katika msiba huo wa Mhe. Silima tokea alipokuwa hospitalini hadi kufariki kwake.

Kifo cha Marehemu Mussa Ame Silima kilitoke tarehe 23 mwezi huu huko katika hospitali ya Muhimbili mjini Dar-es-Salaam alipokuwa akitibiwa baada ya kupata ajali ya gari , Mhe. Mussa alipata ajali juzi ambapo mke wake Bi Mwanakheir Fadhil alifariki hapo hapo kwenye ajali hiyo.

Viongozi wote hao walitoa salamu zao za pole na kumtakia malazi mema peponi maremu ambapo pia, walimwelezea marehemu kuwa alikuwa mchapa kazi, mwadilifu, mpenda watu mtu mwenye nidhamu katika sehemu zake zote za kazi na mtetezi mkubwa wa wananchi wa Jimbo lake na wananchi wote wa Zanzibar na Tanzania kwa jumla.

Walimuelezea marehemu kuwa alifanya kazi kwa moyo wake wote na alikuwa na mashirikiano makubwa na wajumbe wenzake wa Baraza la Wawakilishi pamoja na Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Pamoja na hayo, viongozi hao walisifu mashirikiano makubwa yaliooneshwa katika msiba huo kutoka kwa viongozi wote wa siasa bila ya kujali itikadi zao za vyama.

Marehemu alizaliwa tarehe 15.4.1951 huko Kiboje Mwembeshauri, Wilaya ya Kati, Mkoa wa Kusini Unguja ambapo alipata elimu ya msingi katika skuli ya Kiboje kuanzia mwaka 1961 hadi mwaka 1968 na baadae kuendelea na masomo ya sekondari katika skuli ya Sekondari Uzini mwaka 1969 hadi 1970 na baadae alijiunga na Chuo Cha Ufundi Karume mwaka 1971 hadi 1972.

Marehemu Mussa alianza kazi ya Ualimu mnamo mwaka 1973 na baadae alijiunga na Cho cha Ualimu Nkurumah kwa mafunzo ya Ualimu ngazi ya Stashahada kuanzia mwaka 1981 hadi 1983.

Mbali ya kazi za ualimu, Marehemu aliwahi kushika nyazifa mbali mbali katika masuala ya michezo ikiwa ni pamoja na kuwa Afisa wa Michezo na Mkuu wa Uwanja wa Amaan, Zanzibar baina ya mwaka 2001 na mwaka 2010.

Kwa upande wa shughuli za kisiasa, marehemu amewahi kushika nyazifa mbali mbali katika Jumiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi na kufikia nafasi ya Naibu Katibu Mkuu Zanzibar nafasi aliyoishika hadi kufariki kwake.

Aidha, Mhe. Mussa alikuwa Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi wa Jimbo la Uzini, kupitia Chama Cha Mapinduzi katika uchaguzi Mkuu wa Zanzibar uliofanyika Oktoba mwaka jana.

Pia Marehemu alichaguliwa kuwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano kupitia nafasi tano za Wabunge wanaoingia Bungeni kutoka Baraza la Wawakilishi. Marehemu amewacha watoto watano.