Diwani amkana DC mkutanoni

Baadhi ya ardhi ya Wilaya ya Ludewa

Na Mwandishi Wetu, Ludewa

DIWANI wa Kata ya Ludewa ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa, Monica Mchiro, amemkana hadharani Mkuu wa Wilaya hiyo, Georgina Bundala.
Sakata hilo limetokea mjini Ludewa baada ya mkuu huyo kushindwa kuweka bayana kilichotokea kati ya wananchi na watafiti wa madini walioanza shughuli katika ardhi ya Kata ya Iwela bila taarifa kwa madiwani hali iliyozua hofu na mkanganyiko kwa viongozi na wananchi.
Diwani huyo alifikia hatua hiyo kuweka bayana kwa wananchi baada ya Naibu Kamishna wa Madini Kanda ya Mbeya, John Shija kuweka wazi sheria za madini na jinsi ofisi yake ilivyotekeleza majukumu yake pale ilipotoa leseni ya utafiti katika Kata ya Iwela.
Baada ya ufafanuzi huo, wananchi wengi walilaumu Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Ludewa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya hiyo kwa kushindwa kueleza ukweli kama ilivyobainishwa na Ofisi ya Madini Kanda ya Mbeya.
Taarifa zaidi zinabainisha kuwa wananchi pamoja na viongozi wa kata hiyo walishangaa kuona idadi kubwa ya watu wakiingia katika eneo lao na kuanza shughuli za kutafiti na kuchimba madini bila wao kuwa na taarifa, hivyo kuchukua hatua ya kufuatilia ofisi za wilaya bila kupata majibu ya kuridhisha.
“Ndugu wananchi sisi madiwani wenu tulivyosikia mkanganyo kuhusu watafiti na wachimbaji hao walioko katika Kata ya Iwela, tuliamua kufanya ziara ya kushtukiza lakini tulikuta wahusika wana vibali vyote ikiwemo barua ya Mkuu wa wilaya, jambo hili lilituudhi sana kwani kama walikuwa wanajua kwa nini wasituambie mpaka Halmashauri ikaingia gharama ya kuwasafirisha madiwani wote 35 bila sababu,” alihoji Monica.
Shija aliwaambia wananchi kuwa baada ya watafiti hao kupewa leseni kutoka ofisi ya madini kanda, alimwandikia barua mkuu wa wilaya kuwatambulisha watafiti hao ili utaratibu zifuatwe katika kutekeleza kazi zao katika Kata ya Iwela.
“Kawaida tukishatambulisha mtafiti au mchimbaji kwa mkuu wa wilaya husika, siyo jukumu letu tena kufuatilia mamlaka nyingine, lakini sheria inasema Kamishna wa Madini akishatambulisha ugeni kwa mkuu wa wilaya naye anapaswa kuwatambulisha kwa mkurugenzi na kuwatambulisha katika ngazi zote hadi ulipo mradi,” alibainisha Shija.
Monica alisema Julai 14 mwaka huu, madiwani na wabunge wawili walifanya ziara ya kushitukiza katika Kata ya Iwela kutokana na hofu iliyokuwepo kuwa baadhi ya vigogo wa wilaya wamehusika kuwaleta watafiti na wachimbaji hao kinyemela kwa manufaa yao binafsi.