Lowassa Atoboa Siri ya Richmond, Adai ni Maagizo ya Mamlaka ya Juu

Edward Lowassa kulia akijibu na kutoa ufafanuzi juu ya suala la Richmondi katika mkutano ambao alifunguka juu ya sakata hilo.

Edward Lowassa kulia akijibu na kutoa ufafanuzi juu ya suala la Richmondi katika mkutano ambao alifunguka juu ya sakata hilo.

Edward Lowassa akipunga mkono mara baada ya kuingia katika ukumbi wa mkutano alioamua kutoa ufafanuzi juu ya suala la Richmondi katika mkutano ambao alifunguka juu ya sakata hilo.

Edward Lowassa akipunga mkono mara baada ya kuingia katika ukumbi wa mkutano alioamua kutoa ufafanuzi juu ya suala la Richmondi katika mkutano ambao alifunguka juu ya sakata hilo.


Na Mwandishi Wetu,

WAZIRI Mkuu mstaafu, Edward Lowassa ametua zigo la kashfa ya Richmond iliyosababisha kujiuzulu uwaziri mkuu kwa kueleza jitihada zake alizofanya kabla ya Serikali kuingia mkataba na kampuni hiyo feki iliyoisababishia hasara kubwa nchi. Lowassa ameamua kufunguka hayo jana jijini Dar es Salaam alipoulizwa swali katika mkutano wake na waandishi wa habari kutangaza kukihama Chama Cha Mapinduzi na kujiunga na CHADEMA.

Kiongozi huyo alisema baada ya tishio la kutokea ukame mkubwa kati ya mwaka 2006 na 2007 uliotishia kukatika kwa umeme nchini Serikali ilianza kufanya jitihada za kuweza kupata mashine za ziada za kuzalisha umeme wa dharura utakazo liokoa taifa. Alisema watendaji wa Serikali walianza mara moja kazi ya kupata kampuni itakayofanya kazi hiyo huku yeye akiletewa taarifa kama Waziri Mkuu kipindi hicho.

Alisema baada ya Richmond kupatikana zilianza kutokea tetesi kuwa kampuni hiyo haikuwa na vigezo na kuanza kuhoji kwa watendaji ili kujiridhisha na tetesi hizo dhidi ya kampuni hiyo kabla hata ya kulipwa fedha za kufanya kazi hiyo.

Alisema aliitisha kikao cha watendaji husika akitaka kujiridhisha na tetesi hizo baada ya mazungumzo ya muda mrefu alijulishwa kuwa maelezo yametoka mamlaka ya juu yakitaka Richmond ipewe mkataba bila kujali tetesi hizo.

Alisema baada ya maelekezo hayo aliyoyaita toka mamlaka ya juu Serikalini yeye hakuwa na kipingamizi hivyo kuacha watendaji waendelee na kazi na ndipo kampuni hiyo ilipewa mkataba wa kuzalisha umeme wa dharura wakati wa kipindi kigumu cha ukame nchini, ambao ulizalisha kashfa ya Richmond baadaye.

“…Nilionesha jitihada zangu naamini hata watendaji wakuu wa Wizara husika enzi hizo wanajua, hivyo sihusiki na sakata la Richmond na kama kuna yeyote anayeamini ninahusika anipeleke mahakamani juu ya skendo hiyo…nasema tena sihusiki na nina mikono mweupe kabisa,” alisema Lowassa huku akisisitiza.

Alisema katika sakata la kashfa ya Richmond alijitolea kujiuzulu ili kulinda heshima yake na Serikali jambo ambalo aliliita lilikuwa la uzalendo kwa taifa lake bila kujali muhusika wa suala hilo. Kashfa ya Kampuni ya Richmond ambayo ilichunguzwa na Kamati Maalumu ya Bunge na kusababisha viongozi wengi wa juu Serikalini kujiuzulu wakiwemo Lowassa, ikiwa ni mkataba wa uzalishaji umeme kati ya Serikali kupitia TANESCO na kampuni hiyo uliisababishia hasara kubwa Serikali ya Tanzania na kubaki kwenye historia hadi sasa.