MAOFISA Vijana Nchini wametakiwa kutumia elimu wanayopata katika kuwaendeleza vijana kiuchumi ili kuwawezesha kushiriki katika shughuli za uzalishaji mali. Hayo yamesemwa leo Jijini Arusha na Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Vijana kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, James Kajugusi wakati wa Ufunguzi wa awamu ya kwanza ya mafunzo ya Ujasiriamali na ubunifu.
Bw. Kajugusi alisema kuwa kwa kutambua umuhimu wa kuwaendeleza vijana nchini Wizara kwa Kushirikiana na Chuo cha Uongozi cha Mashariki na Kusini mwa Afrika (ESAMI) wameanzisha mradi unaolenga kuwawezesha vijana kijasiriamali nakiubunifu kwa kupitia mafunzo wanayowapa Maofisa Vijana.
“tunawaomba kushiriki kikamilifu katika mafunzo haya ya ujasiriamali na ubunifu kwa kuwasikiliza wawezeshaji kwa makini kwa dhumuni la kutumia elimu hiyo kuwainua vijana nchini kiuchumi na kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika ujasiriamali,” alisema Kajugusi.
Naye Mkurugenzi wa Ujasiriamali na Ubunifu kutoka Chuo cha Uongozi cha Mashariki na Kusini mwa Afrika (ESAMI), Leon Malisa alisema kuwa dhumuni la mafunzo haya ni kuwajengea uwezo Maofisa Vijana katika eneo la ujasiriamali na ubunifu ili kuwawezesha kuitumia Elimu hiyo kwa vijana vijana nchini kwa kuwawezesha kujiajiri wenyewe.
Aidha Bw. Malisa ametaka vijana nchini kuunda vikundi na kubuni miradi itakayowaendeleza ili Wizara kwa kushirikiana na ESAMI waweze kuwasaidia kujiendeleza ikiwa ni njia moja wapo ya kukabiliana na tatizo la Ajira Nchini.
Akizungumzia kuhusu mafunzo hayo Afisa Vijana toka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Eliackim Mtawa alisema kuwa watatumia mafunzo haya kuwatayarisha vijana kuwa wajasiriamali wazuri na kuwasimamia katika utekelezaji wa Miradi hiyo ili kuwawezesha kushiriki katika uzalishaji mali na kukuza uchumi kupitia ujasiriamali
Mafuzno hayo ya Ujasiriamali na Ubunifu yameandaliwa kwa ushirikiano wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo na Chuo cha Uongozi cha Mashariki na Kusini mwa Afrika (ESAMI)