CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo leo jijini Mwanza kimefanya mkutano mkubwa kupokea kadi za wabunge wawili waliohama toka Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kujiunga na chama hicho. Waliopokelewa rasmi na kutambulishwa katika mkutano huo ulioshirikisha viongozi wa juu wa Chadema ni pamoja na aliyekuwa Mbunge wa CCM Kahama, James Lembeli na Mbunge wa CCM Viti Maalumu, Ester Bulaya ambao wote wamekabidhiwa kadi za Chadema.
Akihutubia baada ya kuwakaribisha vigogo hao wa CCM, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema wabunge hao na wengine wanaojiunga na chama hicho wasamehewe kwa makosa waliyokuwa wakiyafanya ndani ya CCM kwani wameomba na wamekubali kubadilika kuanzia sasa. “…Naombeni wanaMwanza muwasamehe hawa ni Watanzania wenzetu kwa hiyo tuwapokee maana wamekubali kubadilika,” alisema Mbowe akihutubia umati uliohudhuria mkutano huo.
Alisema ndani ya Chadema kuna maadili na misingi yake hivyo kuwataka waiheshimu na kuifuata kama viongozi na wanachama wengine ili kulitumikia taifa. Alisema chama hicho kimepokea majina zaidi ya 1000 ya wanachama wake kutoka majimbo mbalimbali nchini wakiomba kugombea na kuwasihi wawe wastarabu katika kipindi hiki cha kupitia majina hayo kabla ya kupitishwa.
Akizungumzia Umoja wa Katiba uliozaa umoja wa UKAWA alisema mchakato na vikao vinaendelea na viongozi wanaounga umoja huo ili kuhakikisha wanapata mgombea mmoja atakaye gombea nafasi ya urais wa Tanzania akiungwa mkono na vyama vyote vinavyounda umoja huo. Alisema si kazi ndogo kufikia hatima ya mazungumzo hayo hivyo kuwataka wananchi wawaombee ili waweze kufanikiwa kukubaliana na mwisho kumsimamisha mgombea mmoja toka umoja wa UKAWA. Aidha alisema chama hicho “UKAWA tunaendelea na mazungumzo na kushirikiana mazungumzo yetu ni ya msingi katika kukubaliana, tutambue kuna changamoto nyingi lakini tunaomba tumalize salama na kuibuka na mgombea mmoja. Tunafanya mazungumzo haya kwa makini tena kwa kushirikiana na tutamtangaza mgombea wetu hapo baadae, mtafurahi…,” alisisitiza Mbowe.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Chama hicho, Dk Willbroad Slaa alisema Chadema imejipanga kuchukua dola hapo Mwezi Oktoba hivyo wananchi wasiwe na wasiwasi naana wametimia kila idara. “…Si kwamba CCM ikiondoka madarakani itaondoka na Jeshi la Wananchi hapana hili ni Jeshi letu Wananchi hivyo watatuachia…sikwamba watabeba na Jeshi la Polisi na taasisi nyingine za umma jibu ni hapana vyote hivi ni mali ya umma hivyo lazima watuachie hivyo tusihofie jambo lolote,” alisema Dk Slaa akizungumza na Wananchi.
Alisema taarifa zinazoenezwa kwamba yeye na Mwenyekiti Mbowe kwamba hawasalimiani ni za uzushi na hazina ukweli wowote, kwani wao wapo na wanafanya shughuli zao kwa pamoja pasipo na mvutano wowote. “…Habari hizo naombeni mzipuuze hatuna mgogoro wowote mimi na Mwenyekiti wangu,” alisema Dk. Slaa. Alisema chama kinaendelea na mchakato wa kujiandaa na uchaguzi Mkuu na kitakuwa na mikutano kama hiyo Mbeya, Arusha na kumalizia na Dar es Salaam kabla ya kufanyika kwa mkutano mkuu wa taifa wa chama hicho.
Akizungumza baada ya kukabidhiwa kadi ya Chadema, Lembeli aliwataka wananchi kuimaliza CCM kwa kuwanyima kura na kuipigia Chadema kwani chama hicho kimewabeba mafisadi na kuwatelekeza wananchi wake. “…Sasa hivi ni kukata kila kitu, kuanzia wezi wote, mafisadi wote walarushwa, CCM yote sisi ni kukata bila kujali,” alisema kigogo huyo aliyetoka CCM.
Tayari James Lembeli aliyekuwa mbunge wa Kahama kupitia CCM ametangaza kugombea Jimbo hilo la Kahama kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo, Chadema katika uchaguzi unaokuja hapo mwezi Oktoba.