Jairo apokelewa kama mfalme ofisini, gari lake lasukumwa, aimbiwa nyimbo

Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini Bw. David Jairo akisalimiana na baadhi ya wafanyakazi wa Wizara hiyo mara baada ya kuripoti mapema leo asubuhi.

Na Joachim Mushi

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo amepokelewa kama mfalme alipowasili katika Ofisi za Wizara ya Nishati na Madini kurejea kazini baada ya kuchunguzwa na kuonekana hana kosa dhidi ya tuhuma zilizoelekezwa kwake kutokea bungeni.

Jairo aliwasili katika ofisi za wizara hiyo majira ya saa tatu na dakika 16 asubuhi ya leo na kupokelewa na wafanyakazi wa wizara vitengo mbalimbali ambao wanafanyia kazi kwenye jingo hilo ambalo ni makao makuu ya wizara hiyo.

Baada ya kuwasili dev.kisakuzi.com ilishughudia gari la kiongozi huyo likisukumwa na wafanyakazi huku wakiimba nyimbo kadhaa kuonesha bado wanaimani kubwa na kiongozi huyo, kutokana na kutetea maslahi yao zaidi.

Gari la Jairo lilisukumwa hadi eneo ambalo hutumika kama maegesho katika hofisi hizo na baada ya kushuka alionekana akipongezwa na kila mmoja, huku nyimbo zikiendelea kutawala mapokezi hayo.

Wafanyakazi walisikika wakiimba; “tunaimaaaani na Jaiiiiro oyaaaa oyaaaa…Jairo kweli, kweli, kweli kweli kweli kweli Jairooo….,” haya ni baadhi ya maneno ambayo yalikuwa yakiwatoka umati wa wafanyakazi ambao walimpokea.

Wafanyakazi kutoka Idara ya Nishati iliyopo chini ya Wizara ya Nishati na Madini wakilisukuma kwa nyuma gari lililokuwa limembeba Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bw David Jairo mara baada ya kuwasili kwenye Ofisi za Wizara hiyo mapema leo asubuhi.

Hata hivyo Jairo alianza kwa kusalimiana na kila mfanyakazi na baadhi ya maofisa anuai katika ofisi hiyo kabla ya kuingia katika ofisi yake. Baada ya kuingia katika ofisi yake kabla ya kuketi aliinamisha kichwa kama ishara ya kumuomba Mungu kisha kuendelea na shughuli nyingine. Haikujulikana mara moja Jairo alikuwa akiomba nini katika maombi yake.

Ajibu baadhi ya maswali ya wanahabari walioshuhudia mapokezi hayo, Jairo alisema hana kinyongo chochote na wale wote walioibua tuhuma hizo na amewasamehe rasmi, huku akitumia vifungu vya Biblia.

Alisema anafurahi ukweli umebainika baada ya uchunguzi na mikakati yake kwa sasa ni kuchapa kazi ili kupambana na changamoto zinazoikabili Wizara ya Nishati na Madini kwa sasa hasa mgawo wa umeme.

Kurejea kazini kwa Jairo kumekuja baada ya jana Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo kupokea taarifa kamili ya uchunguzi wa tuhuma zilizokuwa zikimkabili Jairo hadi kusimamishwa, kuonekana hakuwa na kosa lolote- hivyo Luhanjo kuamru arejee kazini mara moja.