Sababu za James Lembeli Kuhama CCM Hizi Hapa…
ALIYEKUWA Mbunge wa Kahama James Lembeli, amehamia rasmi Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), akitokea Chama Cha Mapinduzi (CCM). Tukio hilo la kuhama lilifanyika jijini Dar es Salaam leo asubuhi katika Hoteli ya Blue Pearl, Ubungo Plaza ambapo aliambatana na mwanae ambaye alijitambulisha kwa jina Wizilya James.
Ataja YalioAkizungumzia uamuzi wake huo Lembeli alisema amekuwa ndani ya CCM kwa miaka yake yote lakini kutokana na vitendo vinavyofanyika ndani ya chama hicho ameaona akae pembeni. Lembeli alisema, ndani ya CCM ili ufanikiwe kupita michakato yote sahihi ni lazima utoe rushwa au kuiba kura jambo ambalo yeye analipiga vita hivyo kutofautiana na viongozi wa chama ngazi ya Wilaya.
“Ndani ya CCM rushwa imekuwa ibada inasumu kali kuliko ukimwi hivyo nimeshindwa kuvumilia naona Chadema wana viashiria vinavyofanana na mimi ngoja tukafanye kazi,” alisema Lembeli.
Alisema katika harakati za kupata wagombea katika jimbo la Kahama kila mwaka ni lazima rushwa itumike lakini chama kimekuwa kimya na kuwabeba wale watoa rushwa. Mbunge huyo alisema ushahidi wa watu kutoa rushwa hasa katika kipindi hiki umeonekana lakini wahusika wameendelea na hatua zingine bila kukemewa.
“Mimi mwaka 2010 nilikuwa nimekatwa lakini huruma ya Rais Jakaya Kikwete nilirejeshwa sasa nimeona hakuna sababu ya kuendelea kulazimisha kama viongozi hawakutaki,” alisema.
Alisema iwapo angechukua fomu CCM mkakati ambao ulikuwepo ni kumkata kwa kile ambacho wanaamini kuwa amekuwa akisimamia misimamo ambayo ina madhara kwa Serikali. Lembele alisema kutokana na dhana hiyo ni vema aende katika chama ambacho kinaonekana kuwa wabunge wake wanauchungu na nchi yao na sio kubebana kusiko na sababu.
“Kufanya kosa sio kosa lakini kurudia kosa ni kosa kubwa sana hivyo siwezi kurudia kosa la 2010 hivyo huku Chadema ndiko sahihi,” alisema.
Alisema ukiona mwenzako ananyolewa ni vema kujiandaa kwa kutia maji nywele jambo ambalo ameliona na ameamua kufanya hivyo.
“Siwezi kutoa rushwa kwa sababu sijafunzwa hivyo na hata wananchi wa Kahama wanajua kuwa mimi sio mtoa rushwa hivyo ukiwa hutoi rushwa CCM ni ngumu kukubalika jambo ambalo linafanya kuwa rushwa iwe mbaya kuliko ukimwi,” aliongezea.
Akizungumzia kugombea ubunge kupitia Chadema, alisema atafanya hivyo kwani ukweli ni kuwa anakubalika kwa wananchi wote kutokana na misingi yake ya utumishi. Alisema mpaka anafanya uamuzi huo ameshafanya utafiti ambapo anaamini kuwa atashinda tena kwa kishindo kwani wananchi wa jimbo hilo wanamkubali.
Lembeli alisema kimsingi jimbo la Kahama wapinzani wapo tangu yeye akiwa Mbunge, hivyo anaamini kuwa iwapo atafanikiwa kushinda hatapata wakati mgumu kufanya kazi.
“CCM imefanya mambo mengi ambayo kimsingi hayana afya ndani ya chama ukiwa wa kwanza kwa kura ndani ya CCM unakuwa wa mwisho hali ambayo inakatisha tamaa na hilo lilitokea 2010 na Chadema wakapata ushindi,” alisema
Pia alisema amepokea simu na meseji nyingi ambazo kutoka kwa wananchi zinamtaka agombee kupitia chama Chadema hivyo pamoja na ukweli kuwa ni uamuzi mgumu ila hawezi kula matapishi.
Alisema ilimchukua masaa 10 kumuelezea mama yake juu ya uamuzi huo lakini baadae alielewa hivyo kwa sasa ana baraka zote za mama na familia kwa ujumla.