CCM yasema malalamiko ya Rostam hayainyimi ‘usingizi’ Igunga

Katibu Halmashauri Kuu ya Taifa, Itikadi na Uenezi CCM, Nape Nnauye.

Na Joachim Mushi

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema malalamiko aliyoyatoa aliyekuwa Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz pindi anajiuzulu hayawezi kuwanyima ushindi katika uchaguzi mpya unaotarajiwa kufanyika ili kuziba nafasi hiyo baada yam bunge huyo kujiuzulu.

Akizungumza na dev.kisakuzi.com leo katika mahojiano, Katibu Halmashauri Kuu ya Taifa, Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye amesema chama hicho kina utaratibu maalumu wa kushughulikia malalamiko stahili yanapowasilishwa kiutaratibu, hivyo kama mtu atalalama bila utaratibu chama hakitiswi na hali hiyo.

Kada maarufu, Rostam aliwatupia lawama viongozi wa Sekretarieti Kuu ya CCM kuwa wamekuwa wakiupotosha umma na wanachama wa chama hicho katika dhana ya kujivua gamba ilioanzishwa na chama- kwamba wameigeuza kuwalenga wachake akiwemo yeye, jambo ambalo limekuwa likiwachafua wao.

Rostam alisema hakuridhishwa na kampeni hizo zilizokuwa zikiwalenga wazi wazi wanachama na makada maarufu watatu waliokuwa nanafasi za juu za uongozi ndani ya chama hicho, hivyo kuamua kujiengua mwenyewe kwani kampeni hizo zilikuwa zikimchafua kibiashara pia.

Katika mazungumzo yake Nape amesema hakuna kiongozi hata mmoja ambaye aliangaika kujibu tuhuma za Rostam kwani hakuziwasilisha ndani ya CCM kiutaratibu ili zifanyiwe kazi hivyo, hazina madhara yoyote kiushindani kwenye uchaguzi mpya unaotarajia kufanyika Jimbo la Igunga.

Alipoulizwa kuhusiana na vitisho vya baadhi ya wana-CCM ‘wapambe’ wa Rostam Igunga za kugoma kukichagua chama hicho kwa kutokana na malalamiko ya Rostam siku alipokuwa akijiuzulu. Alisema vitisho hivyo haviwezi kukinyima ushindi chama hicho kwani watu waliotoa kauli hizo hawazidi 20, idadi ambayo ni ndogo kwa wanachama wa CCM eneo hilo.

“Waliotoa kauli hizo adharani na wanaojulikana hawazidi 20…Chama Cha Mapinduzi kina wanachama wengi eneo hilo, hivyo kauli kama hizo haziwezi kuwa tatizo la kukinyima ushindi chama,” alisema Nape.

Alipoulizwa kuwa haoni kwamba kitendho cha Rostam kuungwa mkono na idadi kubwa ya wana-CCM Igunga kinaweza kuwa tatizo katika uchaguzi huo alisema; “Unajua sijui unatumia vigezo gani vya kusema yeye ni kipenzi cha wengi (Igunga), kumbuka kwamba ukiangalia takwimu Rostam alishinda takribani kwa asilimia 60, lakini kumbuka kuwa wapo wabunge ambao walishinda hadi kwa asilimia 90 sasa hao utawaitaje.

“Nachoomba tusubiri uchaguzi ufanyike, ninachoamini CCM itashinda tena maana wapinzani tayari wameshindwa uchaguzi kabla ya kuingia kwenye uchaguzi wenyewe…hii ni kutokana na ugawanyiko ulioonekana kati yao,” alisema Nape.