Mambo yageuka Tripoli, waasi warudishwa nyuma na Jeshi la Gaddafi

Mapigano Tripoli

MAPIGANO yanaendelea kati ya pande mbili muhimu Mji Mkuu wa Libya, Tripoli, kwa siku ya tatu mfululizo huku wapiganaji waasi wakipambana na vikosi vinavyomtii Kanali Muammar Gaddafi.

Milio ya risasi na milipuko imekuwa ikisikika karibu na hotel inayotumiwa na vikosi vya serikali pamoja na eneo la makazi ya kiongozi wa Libya ya Bab al-Aziziya.

Usiku mzima, mtoto wa Kanali Gaddafi, Saif al-Islam alionekana hadharani, ikipinga ripoti kuwa alikuwa amekamatwa. Saif al-Islam, ambaye awali waasi walidai wamemkamata, amejitokeza katika hoteli moja inayoshikiliwa na wafuasi wa Kanali Gaddafi.

Mwandishi wa BBC, Matthew Price amezungumza na Saif al-islam na kusema kuwa anaonekana kuwa mchangamfu na mwenye shauku. Saif al-Islam amesema waasi wameingia kwenye ”mtego” mjini Tripoli na kwamba wanajeshi wanaomuunga mkoni Kanali Gaddafi walikuwa ”wamevunja uti wa mgogo wa waasi hao”.

Waasi wanaopigana kuudhibiti Mji Mkuu wa Libya, Tripoli, wamerudishwa nyuma na wanajeshi wanaomuunga mkono Kanali Muammar Gaddafi. Lakini wakati mapigano yanapoendelea katika maeneo mbalimbali ya mji, msafara wa waasi kutoka mashariki mwa nchi ulirudishwa nyuma.

Bado hajulikani alipo Kanali Gaddafi. Jumapili iliyopita waasi walidai kuwa walikuwa wamemkamata Saif al-Islam, pamoja na familia yake. Hata hivyo, bado Kanali Gaddafi hajulikani alipo. Nyumba yake inalindwa na wapiganaji wanaomtii.

Waasi hao walioingia mjini Tripoli jumamosi iliyopita walikaribishwa watu waliokuwa wakisheherekea katika bustani ya Green Square wakati walipowasili siku ya jumapili. Waasi hao wamesema kuwa wameweka vizuizi katika sehemu mbalimbali za mji lakini wanakabiliwa na upinzani mkali katika baadhi ya maeneo.

Kamanda wa waasi amesema wanadhibiti asilimia 90 ya Mji wa Tripoli. Kiongozi wa Baraza la Mpito la kitaifa (NTC), Mustafa Abdel Jalil, amesema wakati wa ushindi halisi utakuwa pale watakapo mkamata Kanali Gaddafi.