Na Joachim Mushi
MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh amesethibitisha tuhuma zilizotolewa Bungeni Julai 18, mwaka huu, dhidi ya Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo si za kweli na hivyo katibu huyo hana kosa.
Taarifa hiyo imetolewa leo Dar es Salaam kwa waandishi wa habari na Katibu Mkuu Kiongozi, Phillemon Luhanjo pamoja na Utouh katika mkutano uliofanyika Ikulu. Kutokana na matokeo hayo kumsafisha Jairo, Luhanjo ameamuru Katibu Mkuu huyo kurejea kazini maramoja.
Akifafanua kuhusiana na uchunguzi huo, Utouh amesema ukaguzi maalum umebaini idadi ya taasisi zilizopelekewa barua za kuchangia gharama za kuwasilisha bungeni Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini ni nne tu na si 20 kama tuhuma zilivyodai awali.
Aidha amefafanua kuwa fedha zilizochangishwa ni sh. milioni 149, 797, 600 tu, huku akiainisha kuwa Idara ya Uhasibu ya Wizara ilichangia sh. milioni 150, 720, 000 kwa ajili ya posho za vikao vya kazi katika uandaaji wa uwasilishaji wa bajeti ya wizara. Idara ya Mipango ilichangia sh. milioni 278, 081, 500.
“…jumla ya michango yote iliyochangishwa ni sh. milioni 578, 599, 100 na siyo bilioni moja iliyotajwa kwenye tuhuma. Taasisi moja yaani Ewura haikutuma mchango wake GST kama ilivyokuwa imeagizwa bali ilijitolea kugharamia chakula cha mchana cha sh. milioni 3.6 kilicholipwa kwa kampuni ya African Conference Centre Ltd.
“Ewura pia ililipia gharama za tafrija iliyofanyika Julai 18, 2011 jioni kwenye Ukumbi wa St. Gasper uliopo Dodoma kwa gharama ya sh. Milioni 6.1, pamoja na ukweli kwamba bajeti hiyo haikupita lakini tafrija ilifanyika kwa kuwa taratibu zote zilikwishafanyika, hivyo fedha lazima zingelipwa.
“Taasisi ya Rural Energy Agency (REA) ilitoa sh. milioni 50, 000, 000 kama ilivyoombwa, Tanesco sh. milioni 40, 000, 000, TPDC sh. milioni 50, 000, 000, Ewura sh. milioni 40, 000, 000, Idara ya Uhasibu ya Wizara sh. milioni 149, 797, 600 na Idara ya Mipango sh. milioni 428, 801, 500. Jumla kuu ilikuwa sh. milioni 578, 599, 100 na si bilioni moja,” aliongeza.
Amesema; “…pamoja na mahojiano yaliyofanyika na mapitio ya nyaraka mbalimbali, ukaguzi maalum haukuweza kuthibitisha tuhuma hizo za kiasi cha fedha zilizochangwa cha sh. bilioni moja kutoka kwenye taasisi 20 kama ilivyorekodiwa kwenye “Hansard” ya Bunge Julai 18, 2011,” alisema CAG Utouh.
Awali baada ya kuibuka kwa tuhuma hizo, Katibu Mkuu Kiongozi ambaye ni mamlaka ya nidhamu ya Katibu wa Wizara ya Nishati na Madini Julai 21 mwaka huu aliamua ufanyike ukaguzi maalum na hivyo kumwandikia CAG barua na kufanya kazi hiyo.