Kijiji cha Mahongole Njombe kujengewa Soko

Baadhi ya wakulima wa Kijiji cha Mahongole mkoani Jombe wakikokota baskeli zenye nyanya kutafuta masoko ya bidhaa hizo.

Na Mwandishi Wetu, Njombe

WAKULIMA wa nyanya katika Kijiji cha Mahongole kilichopo mkoa mpya wa Njombe wameahidiwa kujengewa soko na mradi wa Muunganisho Ujasiriamali Vijijini (MUVI), ili kuwaondolea kero ya kusafiri umbali mrefu kutafuta masoko.

Akizungumza kwa niaba ya Mratibu wa Mradi huo mkoani hapa, Ofisa Mradi, Christopher Mkondya, amesema soko hilo ambalo kwa kiasi kikubwa litagharamiwa na mradi huo litakuwa mhimili mkubwa kwa wakulima wa nyanya kwani wamekuwa wakisafiri umbali wa kilometa zaidi ya 20 kufuata soko.

Wakulima hao ambao husafirisha nyanya kwenda Soko la Makambako, wameunganishwa katika vikundi ili waweze kushirikiana katika utekelezaji na usimamizi wa soko.

Mkondya ameongeza kuwa soko hilo litakuwa chini ya wanakijiji wa Mahongole, lakini wakulima wengine wataruhusiwa kuuzia nyanya zao kwa kulipia ushuru utakaosadia uendeshaji wa soko.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakulima wa nyanya wamesema; kutokana na kusafiri umbali mrefu, bidhaa zao zimekuwa zikishuka thamani.

“Tunasafiri umbali mrefu kupeleka nyanya hususani, wanakijiji wa Mahongole, tunakokota baiskeli ikiwa na nyanya umbali wa zaidi ya kilometa 20 tunafika sokoni tukiwa tumechoka hali ambayo huwafanya wanunuzi kutumia uchovu wetu kutugandamiza,” alisema mmoja wa wakulima.

Tayari hatua za awali za ujenzi wa soko hilo zimenza na soko linatarajiwa kukamilika hivi karibuni, jambo ambalo litawaondoa wakulima kutoka kwenye mateso ya usafirishaji wa nyanya kuelekea sokoni.

Naye Ofisa Habari wa mradi huo mkoani humo, William Macha amesema ujenzi wa soko ni utekelezaji wa lengo kuu la mradi ambalo ni kuongeza mnyororo wa ongezeko la thamani ya mazao.

Aidha ameongeza kuwa kupitia mbao za matangazo katika kata zao, redio washirika, Upland Fm na Country Fm wakulima watakuwa wakipata taarifa mbalimbali za uzalishaji pamoja na masoko.

Macha amewataka wanavikundi wa Mahongole kuonesha mshikamano wa hali ya juu katika kusimamia vizuri ujenzi wa soko na uendeshaji pindi litakapokamilika. Meongeza kufanikisha ujenzi huo wanakijiji watachangia kiasi fulani cha gharama ikiwa ni fedha taslimu pamoja na nguvu kazi.