NI fainali leo pale vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vitakapompitisha mgombea wake urais atakayepambanishwa na yule wa CCM, Dk John Magufuli aliyepitishwa Dodoma juzi.
Fainali hiyo ndani ya Ukawa inatarajiwa kuhitimisha mvutano uliokuwapo baina ya Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba ambaye tayari amechukua fomu kuwania urais ndani ya umoja huo na mgombea anayetajwa na Chadema, Dk Willibrod Slaa. Mwingine aliyechukua fomu katika umoja huo ni Dk Kahangwa wa NCCR-Mageuzi.
Yeyote atakayeibuka katika mpambano huo na kutangazwa rasmi leo, atakwenda kushindana katika fainali nyingine dhidi ya mgombea wa CCM katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 25. Wanaopewa nafasi ni Dk Slaa aliyegombea urais kwa mara ya kwanza mwaka 2010 na kutoa upinzani mkali kwa Rais Jakaya Kikwete na Profesa Lipumba ambaye amejaribu bahati yake mara nne, 1995, 2000, 2005 na 2010 na sasa akitaka kujaribu kwa mara ya tano.
Wawili hao wameibua mvutano ndani ya vikao vya Ukawa na wajumbe wengi walikuwa wanaipa nafasi Chadema kusimamisha mgombea urais wa Muungano baada ya CUF kupewa nafasi ya kusimamisha mgombea urais Zanzibar. Jumamosi iliyopita, kamati ya viongozi ya wakuu wa vyama vinavyounda umoja huo, NCCR-Mageuzi, Chadema, NLD na CUF ilikutana asubuhi na jioni kutoa tathmini ya walichokubaliana mbele ya wabunge wote na viongozi wa vyama hivyo kuwa mgombea wao atatangazwa leo.
Akitangaza uamuzi huo, Profesa Lipumba aliwaeleza waandishi wa habari kwamba kuna mambo ya kujadiliana baina ya vyama hivyo ila hayawezi kuleta matatizo, kwamba wapo pamoja na watatoa majibu ya pamoja. Takriban wiki mbili sasa, viongozi wa Ukawa wamekuwa na mjadala mzito kuhusu kugawana majimbo ambayo mpaka sasa wamekubaliana kwa asilimia 97 na kushindwa kuafikiana kuhusu urais kutokana na mvutano kati ya Chadema na CUF.
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe aliliambia gazeti hili jana kuwa kikao cha leo kipo palepale na kusisitiza kuwa bado wanaendelea na mazungumzo.
“Watanzania wasubiri kesho (leo) tutawaleleza kilichoafikiwa. Unajua kwenye siasa saa 24 zinaweza kuwa miezi 24. Siasa ni siasa na kila kitu kinawezekana katika siasa,” alisema.
“Kama tumeshawaambia watu kesho (leo) ndiyo tutazungumza, itabaki kuwa hivyo. Leo (jana) hatuwezi kusema chochote. Unajua tuna vitu vingi tunaendelea kuvikamilisha kwa sasa, tuvute subira na kila kitu tutakiweka wazi kesho,” alisema Mbowe.
Leo kabla ya kumtaja mgombea wa urais, viongozi wa Ukawa watakuwa na kikao cha majadiliano ambacho kitatoa mwelekeo wa umoja huo huku taarifa kutoka ndani ya vyama hivyo zikieleza kuwa mwafaka bado haujapatikana.
Taarifa zaidi zinaeleza kuwa licha ya mazungumzo yanayoendelea kufanywa na viongozi wa Ukawa, hadi jana mchana bado kulikuwa na wingu zito juu ya nani atakayepeperusha bendera ya umoja huo katika Uchaguzi Mkuu.
“Kesho (leo) tutaanza na kikao kwanza. Sidhani kama kutakuwa na mabadiliko sana ila tunasubiri kuona kitakachoendelea katika kikao. Baada ya hapo nadhani tutakuwa katika hatua nzuri ya kuona tunakwendaje katika Uchaguzi Mkuu,” zilieleza taarifa hizo.
Zilieleza kuwa hatua ya CCM kumpitisha Dk Magufuli kugombea urais imeibua changamoto mpya ndani ya Ukawa kutokana na rekodi yake ya utendaji kazi na kukubalika kwake katika jamii.
“Tunapaswa kujipanga kwa kuweka wagombea wazuri na sahihi kuanzia udiwani, ubunge na urais,” zilifafanua taarifa hizo.
Taarifa za ndani za kikao cha Ukawa cha Jumamosi, zinaeleza kuwa mvutano ulikuwa mkali kutokana na Profesa Lipumba kuungwa mkono na baadhi ya viongozi wa CUF na NCCR baada ya kutoa hoja ya kutaka apitishwe kugombea urais.
Zinaeleza kuwa jambo hilo liliibua mvutano na kupingwa na viongozi wengine wa vyama vinavyounda Ukawa kwa maelezo kuwa nafasi hiyo anapaswa kupewa Dk Slaa kwa kuwa anakubalika zaidi Tanzania Bara na kwamba hata katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 alimtikisa mgombea wa CCM, Rais Jakaya Kikwete. Ilielezwa kwamba baadhi ya viongozi wa CUF, wakiwamo kutoka Zanzibar wametoa baraka kwa Dk Slaa kugombea, lakini kikwazo kimebaki kwa wenzao wachache wanaomuunga mkono Profesa Lipumba.
Lowassa na Ukawa
Wakati hali ikiwa tete ndani ya Ukawa, jana zilisambaa taarifa katika mitandao ya kijamii zikidai kwamba Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa yupo katika maandalizi ya kujiunga na Chadema baada ya CCM kutompitisha kuwa mgombea wake. Taarifa hizo zinaeleza kuwa hali hiyo imezua sintofahamu ndani ya Chadema na kuelezwa kuwa Dk Slaa amepinga uamuzi huo na kutoa msimamo kuwa iwapo Lowassa atajiunga na chama hicho, atarudisha kadi yake.
Akitolea ufafanuzi juu ya jambo hilo, Mbowe alisema; “Hakuna kitu kama hicho, hizo ni taarifa za umbeya tu na katika mitandao ya kijamii. Chadema hakuna migogoro wala jambo linalofanana na hilo.”
Tangu CCM impitishe Dk Magufuli na kuachana na Lowassa ambaye hakufanikiwa kuingia hata katika tano bora, kumeibuka taarifa kuwa kiongozi huyo atakihama chama hicho na kujiunga na vyama vya upinzani, huku Chadema na Chama cha Wazalendo (ACT) vikitajwa zaidi.
Moto wa taarifa hizo ulikolezwa jana baada ya Lowassa kuitisha mkutano na waandishi wa habari nyumbani kwake Masaki, ikidhaniwa kuwa alikuwa akitaka kuzungumzia hatima yake ya kisiasa na mchakato wa CCM kumpata mgombea wake wa urais, lakini akauahirisha bila maelezo yoyote wala kutaja utafanyika lini.
CHANZO: http://www.mwananchi.co.tz/