Na Joachim Mushi
TFF imeshindwa kumpa leseni Castory Mumbara ambaye ameombewa usajili katika timu ya Toto Africans kutokana na kutokuwa na Hati ya Uhamisho ya Kimataifa (ITC), ambayo inatakiwa kutolewa kupitia mfumo wa mtandao wa Transfer Matching System (TMS).
Taarifa hiyo imetolewa leo Dar es Salaam na TFF, kupitia kwa Ofisa Habari wake, Boniface Wambura alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari.
“Ikumbukwe kuwa Mumbara alikuwa akichezea timu ya Himalayan Sharpa ya Nepal ambapo alikwenda huko baada ya TFF kumpatia ITC. Hivyo ili aichezee Toto Africans, klabu hiyo ilipaswa kumuombea hati hiyo kupitia mtandao wa TMS baada ya kufanya mawasiliano na Himalayan Sharpa,” alisema Wambura.
Wambura alisema muda wa usajili ulimalizika Julai 31 mwaka huu, hivyo Toto Africans kwa sasa haiwezi kumtumia mchezaji huyo badala yake inatakiwa kusubiri dirisha dogo la usajili litakapofunguliwa tena Novemba mwaka huu.
Ameongeza kuwa, TFF iliendesha mafunzo ya kutumia mfumo wa TMS kwa watendaji wote wa klabu za Ligi Kuu ikiwemo Toto Africans.
Wakati huo huo, mechi hiyo namba 103 ya mchujo kuwania tiketi ya Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika zitakazofanyika mwakani Equatorial Guinea na Gabon itachezwa nchini Septemba 3 mwaka huu.
Akizungumzia suala hilo leo, Wambura amesema; “Bado tunasubiri majibu ya ombi letu Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo la kuturuhusu kutumia Uwanja wa Taifa kwa ajili ya mechi hiyo.
Ameongeza kuwa, mwamuzi msaidizi John Kanyenye wa Tanzania ni miongoni mwa waamuzi 32 (waamuzi wa kati na wasaidizi) walioteuliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) kuchezesha michezo ya All Africa Games itakayofanyika Maputo, Msumbiji kuanzia Septemba 3-18 mwaka huu.
“Kati ya hao, 16 ni wanaume na 16 ni wanawake. Kanyenye ni mmoja kati ya waamuzi watatu kutoka ukanda wa CECAFA- Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati walioteuliwa kuchezesha michezo hiyo. Wengine ni mwamuzi wa kati wa kike kutoka Uganda, Nabikko Ssemambo na mwamuzi msaidizi wa kike kutoka Ethiopia, Trhas Gebreyohanis.” Amesema Wambura.