Na Mwandishi Wetu, Dodoma
MGOMBEA wa Chama Cha Mapinduzi kwa nafasi ya urais katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu, Dk. John Pombe Joseph Magufuli amemteuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano) Bi. Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea mwenza wa Nafasi hiyo. Dk. Magufuli amemteuwa Bi. Samia kuwa mgombea mwenza leo mjini Dodoma ikiwa ni muda mfupi baada ya kutangazwa kushinda nafasi hiyo ya kupeperusha bendera ya CCM.
Bi. Samia ambaye ni Waziri wa Muungano na Mtanzania mwenye asili ya Zanzibar anakuwa ni mgombea mwenza wa kihistoria mwanamke kugombea nafasi hiyo ndani ya CCM. Kama Chama Cha Mapinduzi pia kitafanikiwa kushinda nafasi hiyo atakuwa ni mwanamke wa kwanza kihistoria kushika nafasi kubwa katika Serikali ya Tanzania.
Akiwahutubia wajumbe wa Mkutano Mkuu Maalum wa CCM mara baada ya kutangazwa, Dk. Magufuli ambaye ni mbunge wa Jimbo la Chato (CCM) alisema anawashukuru wajumbe hao kwa kuonesha imani kubwa kwake na kumchangua kwa ushindi wa kishindo kupeperusha bendera ya Chama hicho katika Uchaguzi Mkuu wa Tanzania.
alisema anaahidi kufanya kazi kama mtumishi na atawatumikia wajumbe na Watanzania kwa karibu na uadilifu mkubwa endapo atafanikiwa kushinda nafasi hiyo. Dk. Magufuli ambaye alionekana kukubalia kiasi kikubwa na wajumbe wa mkutano huo maalumu alishangiliwa kwa kiasi kikubwa na ameungwa mkono na wagombea wote alioingia nao kwenye ushindani hatua ya tatu bora. Mgombea huyo ameshinda nafasi hiyo baada ya kupata kura 2104 kati ya kura 2422 za wajumbe wote zilizopigwa.
Akifunga mkutano huo maalum mjini Dodoma leo, Mwenyekiti wa Chama hicho, Rais Jakaya Kikwete alisema anaimani kubwa na mgombea wa CCM Dk. Magufuli kutokana na utendaji wake na kumuita ni zaidi ya ‘jembe’ tingatinga kwa utendaji kazi. Alisema atahakikisha anazunguka kumnadi mgombea huyo pamoja na makada wengine wa chama ili kuhakikisha chama chao kinapata ushindi mkubwa.
CCM inatarajia kumtambulisha mgombea wake katika mkutano wa kwanza utakaofanyika Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma leo na siku ya Jumanne itamtangaza mjini mgombea huyo jijini Dar es Salaam.