Dk. Magufuli Rasmi Mgombea wa CCM Urais Oktoba 2015

Dk. John Pombe Joseph Magufuli mgombea Urais wa CCM 2015.

Dk. John Pombe Joseph Magufuli mgombea Urais wa CCM 2015.

Mgombea Urais wa CCM 2015, Dk. John Pombe Joseph Magufuli (kulia) akisalimiana na mgombea mwenzake aliyechujwa katika hatua ya tano bora, Benard Membe.

Mgombea Urais wa CCM 2015, Dk. John Pombe Joseph Magufuli (kulia) akisalimiana na mgombea mwenzake aliyechujwa katika hatua ya tano bora, Benard Membe.


Wagombea wa CCM walioingia Tatu Bora.

Wagombea wa CCM walioingia Tatu Bora.


Wagombea wa CCM walioingia Tano Bora.

Wagombea wa CCM walioingia Tano Bora.


Na Joachim Mushi

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimemaliza mchakato wa kumpata mgombea wake atakayepeperusha bendera yake kwenye kinyang’anyiro cha Uchaguzi Mkuu wa Oktoba baada ya kumchagua, Dk. John Pombe Joseph Magufuli kuwa mgombea wao wa nafasi ya urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Dk. Magufuli ambaye ni mbunge wa Jimbo la Chato (CCM) lililoko Mkoa wa Geita na pia Waziri wa Ujenzi wa Serikali ya Tanzania amechaguliwa rasm baada ya kuwashinda wagombea wenzake wawili walioingia tatu bora katika Mkutano Mkuu Maalum wa CCM. Mgombea huyo ameshinda nafasi hiyo baada ya kupata kura 2104 kati ya kura za wajumbe wote 2422, ambapo kura sita ziriharibika katika uchaguzi huo.

Wapinzani wa Magufuli walioingia naye tatu bora ni pamoja na Dk. Asha-Rose Migiro aliyepata kura 59 sawa na asilimia 2.4 za wajumbe wote wa Mkutano Mkuu, pamoja na Balozi Amina S. Ali aliyepata kura 253 sawa na asilimia 10.5 katika uchaguzi huo. Kwa matokeo hayo sasa Dk. Magufuli ambaye ni kati ya wagombea wa nafasi hiyo ambao hawakuwa na mbwembwe tangu awali kwenye mchakato wa kutangaza nia ya kugombea ndani ya chama hicho ukilinganisha na wagombea wenzake ndani ya CCM ametangazwa rasmi na Mwenyekiti wa CCM Taifa, Dk Jakaya Kikwete mjini Dodoma.

Kihistoria Magufulia alizaliwa Oktoba 29, 1959 wilayani Chato Mkoani Kagera. Alipata elimu yake ya Msingi Mwaka 1975 hadi 1977 katika Shule ya Msingi Katoke, Biharamulo mkoani Kagera na baadaye elimu ya Sekondari Mwaka 1977 hadi 1978 katika Shule ya Sekondari Lake, Mwanza. Alipata mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Mpwapwa mkoani Dodoma kati ya Machi 1984 hadi Juni 1984. Januari 1984 hadi Machi 1984 alikuwa JKT Makuyuni, Arusha na baadaye JKT Makutupora, Dodoma, Julai 1983.

Alianza kupata elimu yake cha Chuo Mwaka 1981 hadi 1982 katika Chuo cha Mkwawa akisomea ualimu ngazi ya diploma masomo ya Kemia na Hisabati na baadaye shahada ya kwanza Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1985 hadi 1988 akichukua masomo ya Kemia na Hisabati. Mwaka 1991 hadi 1994, alisoma tena Shahada ya Uzamili (Kemia) katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na baadaye Chuo Kikuu cha Salfordnchini Uingereza.

Uzoefu wa kazi; Mwaka 2010 – hadi sasa amekuwa Waziri wa Ujenzi na Mwaka 2008 hadi 2010 alikuwa Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Samaki na Mbunge wa Biharamulo Mashariki (Chato). Mwaka 2005 hadi 2008 alikuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi. Mwaka 2000 hadi 2005 akiwa Waziri wa Ujenzi, Mwaka 1995 hadi 2000 alikuwa Naibu Waziri wa Ujenzi.

Amewahi kufanyakazi kama Mkemia wa Chama cha Ushirika cha Nyanza Cooperative Union (Ltd.), Mwanza mwaka Mwaka 1989 hadi 1995 na mwalimu katika Shule ya Sekondari Sengerema mnamo mwaka 1982 hadi 1983 akifundisha masomo ya Kemia na Hisabati). Dk. Magufuli pia amepata tuzo mbalimbali za ndani na nje ya nchi na ameandika vitabu na majarida mbalimbali. Ameoa na ana watoto.