Yanga, Simba zabadili viwanja Ligi ya Vodacom

Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura

Na Mwandishi Wetu

TIMU za Simba na Yanga zote za jijini Dar es Salaam zimefanya mabadiliko ya viwanja zitakavyovitumia katika Ligi Kuu ya Vodacom baada ya Serikali kuufunga Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ambao ulikuwa utumiwe na timu hizo.

Marekebisho hayo yametolewa leo na Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa Wambura sasa timu ya Yanga ya Dar es Salaam itautumia Uwanja wa Jamhuri, mjini Morogoro, huku Simba ya jijini Dar es Salaam ikiuchukua Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga kama uwanja wake wa nyumbani katika ligi hiyo.

Awali timu za Yanga na Simba zilikuwa zimeruhusiwa kutumia uwanja wa Taifa wa Jijini Dar es Salaam kwa ajili ya mechi za Ligi Kuu ya Vodacom, ambao umefungwa na Serikali kwa ajili ya marekebisho hivyo kuzitaka timu hizo kutafuta viwanja vipya.

“Simba imehamia Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga wakati Yango iko Uwanja wa Jamhuri, mjini Morogoro. Licha ya timu hizo kupata viwanja vipya ratiba itabaki kama ilivyotolewa awali,” alisema Wambura katika ufafanuzi wake.

Aidha aliongeza kuwa kutokana na mabadiliko hayo ratiba inasomeka kuwa Septemba 7 mwaka huu Coastal Union Vs Moro United (Mkwakwani) na pia Simba Vs Villa Squad (Mkwakwani).

Hata hivyo aliongeza kuwa mechi kati ya Simba na Villa Squad imesogezwa mbele kwa siku moja, ambapo sasa itachezwa Septemba 8 mwaka huu kwenye uwanja huo huo.