Na Mwandishi Wetu
KITENGO cha Utafiti cha Magonjwa ya Binadamu cha Taifa (NIMR) leo kimezinduwa kitabu cha utafiti kitakachosaidia uboreshaji mfumo wa huduma za afya, uandaaji wa ajenda za kitafiti juu ya utafiti wa mifumo wa afya wa magonjwa ya kifua kikuu na maleria na pamoja na magonjwa ya kitropiki (NTD).
Akizinduwa utafiti huo leo jijini Dar es Salaam kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Donan Mbando mwakilishi wa katibu mkuu huyo alisema utafiti huo umefanywa kwa nguvu ya pamoja kati ya Shirika la UNDP, Shirika la Afya Duniani (WHO), Watu wa Japani na Serikali ya Tanzania kupitia Kitengo cha Utafiti cha Magonjwa ya Binadamu cha Taifa (NIMR).
Alisema kitabu hicho cha utafiti kimeangalia masuala gani muhimu yanayotakiwa kufanyiwa utafiti, kutambua na kutatua vitu vinavyotatiza mfumo wa afya kutotoa huduma inayostahiki na kwa mafanikio kwa wagonjwa au walengwa.
“..’Kitabu kimeangalia ni masuala gani muhimu ya kuboreshwa ili kusaidia kuboresha mfumo wa huduma za afya, huku ukipewa jina la ‘Uandaaji wa ajenda ya kitafiti juu ya utafiti wa mifumo wa afya wa magonjwa, kifua kikuu na maleria na magonjwa ya kitropiki ambayo yalikuwa hayapewi kipaumbele hapo awali,” alisema Dk. Mbando katika hotuba yake iliyosomwa na mwakilishi wake.
Alisema licha ya changamoto zinazoikabili sekta ya afya, mpango wa afya wa taifa umebaini vikwazo vitatu vikuu ambavyo vimekuwa changamoto katika kufikia malengo ya utoaji huduma bora kiufasaha ambapo alivitaja vikwazo hivyo hivyo kuwa ni pamoja na miundombinu ya afya, mgawanyiko wa watumishi wa afya na mfumo wa uongozi wa idara ya afya. Aliongeza kuwa pamoja na hayo suala zima la kikwazo cha upatikanaji wa bajeti ya kutosha katika eneo zima la shughuli za afya.
Hata hivyo licha ya changamoto hizo alisema Serikali imepata mafanikio kwa ujumla katika sekta ya afya, kwani kumekuwepo na mafanikio katika kupunguza vifo vya watoto wachanga na vifo kwa wajawazito, pia kupungua kwa kiasi kikubwa kwa vifo kwa watoto chini ya miaka 5 ambapo vifo vimepungua kutoka 137/1000 hadi 81/1000. fungua
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Kitengo cha Utafiti cha Magonjwa ya Binadamu cha Taifa (NIMR), Dk. Julias Masaga akizungumza alisema mradi huo wa utafiti umefanywa sasa ili kuangalia kitu gani kipya ambacho kinaweza kusaidia kuzuia magonjwa ya kifua kikuu (TB), maleria na pamoja na magonjwa ya kitropiki (NTD).
“…Tumetafuta njia mpya ambazo zitasaidia kuzuia, watafiti wetu wamekaa kwa makundi matatu wakaangalia ni matatizo gani yanayokwamisha huduma hizi, lengo likiwa ni kupunguza matatizo ya kiafya na pia kuangalia namna ya kutatua. Tumefanya sasa ili kuangalia kitu gani kipya ambacho kinaweza kusaidia kuzuia haya magonjwa,” alisisitiza Dk. Masaga katika hotuba yake.
Alisema pamoja na tafiti hizo hali halisi inaonesha ugonjwa wa maleria kwa sasa unapungua ikiwa ni kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo pia mabadiliko ya tabia nchi, huku ugonjwa wa kifua kikuu ukichochewa na ugonjwa wa Ukimwi. “Awali tulifanikiwa kwenye kifua kikuu ila kwa sasa umeanza kurudi ukichangiwa na ugonjwa wa Ukimwi na tafiti kama hizi zinatusaidia zaidi namna ya kukabiliana,” alisema Dk. Masaga akizungumza na wana habari mara baada ya uzinduzi wa kitabu cha utafiti.