Rais Kikwete Alivunja Bunge, Asema Nitawa-Miss Watanzania

Rais Jakaya Kikwete akilihutubia Bunge kabla ya kulivunja.

Rais Jakaya Kikwete akilihutubia Bunge kabla ya kulivunja.


RAIS wa Tanzania, Jakaya Kikwete amelivunja bunge la jamhuri ya muungano wa Tanzania mjini Dodoma mara baada ya kulihutubia ikiwa ni hatua za kumalizia utawala wake kabla ya kukabidhi kijiti kwa rais atakayechaguliwa hapo baadaye Oktoba.

Katika hotuba yake ametaja mafanikio lukuki ambayo yamepatikana ndani ya utawala wake huku akijinasibu kutekeleza asilimia 88 ya ahadi zake kwa Watanzania. “…Tulipanga kufanya mengi na tumefanikiwa mengi, lakini hatukuweza kuyamaliza yote kwa sababu ya changamoto mbalimbali na kubwa zaidi ni uhaba wa rasilimali fedha na wakati mwingine rasilimali watu na vitendea kazi. Hata hivyo tumeweza kutekeleza zaidi ya asilimia 88 ya ahadi zetu zilizomo kwenye Ilani za Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi na mipango ya Serikali,” alisema Rais Kikwete katika hotuba yake.

Alisema changamoto za nchi haziishi kila siku zinaibuka mpya na kila ikimalizika moja inazaa nyingine hivyo utawala wake umejitahidi kushughulikia kadaa. “..Hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa baba wa taifa ambaye naye hakumaliza changamoto zote, ndivyo ilivyokuwa kwa Mzee Mwinyi na hivyo ndivyo alivyoniachia Rais Mkapa. Nami namwachia anayekuja, naye afanye yake na yatakayobakia atamwachia atakayemfuatia. Jambo linalonipa faraja ni kuwa nami nimetoa mchango wangu kwa maendeleo ya nchi yetu na watu wake.” Anasema Kikwete.

Aidha aliwashukuru Watanzania kwa kumuamini na kumchagua mara mbili kuwa kiongozi wa nchi. “..Nawashukuru kwa kuniunga mkono wakati wote wa uongozi wangu. Mmenipa heshima kubwa ambayo sitakaa nisahau maishani mwangu. Ninamaliza kipindi changu cha uongozi nikiwa nawapenda sana na nitaendelea kuwapenda mpaka siku Mwenyezi Mungu atakaponiita.

“Nitawa-miss kama mtumishi na kiongozi wenu mkuu lakini tutakutana kwa urahisi zaidi nikiwa raia. Baada ya hotuba yangu ndefu, sasa natangaza kuwa Bunge la 10 limevunjwa rasmi, lakini linabakia kuwa hai mpaka tarehe itakayotangazwa rasmi kwenye Gazeti la Serikali kwa mujibu wa Katiba.
Mungu ibariki Afrika, Mungu ibariki Tanzania..,” alisema Rais Kikwete katika hotuba yake.
Soma hotuba nzima ya Rais Kikwete katika kurasa za mtandao huu.