Mawaziri wa Zamani, Mramba na Yona Wahukumiwa Kifungo Jela

Basir Mramba (kulia), Gray Mgonja (kushoto) na Daniel Yona wakiwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es salaam.

Basir Mramba (kulia), Gray Mgonja (kushoto) na Daniel Yona wakiwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es salaam.


Na Mwandishi Wetu

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam imewahukumu kwenda jela miaka mitatu kila mmoja aliyekuwa waziri wa zamani wa Fedha, Bazil Pesambili Mramba na aliyekuwa Waziri wa zamani wa Nishati na Madini, Daniel Yona baada ya kukutwa na hatia ya uhujumu uchumi, matumizi mabaya ya ofisi na kuisababishia Serikali hasara ya sh. bilioni 11.7.

Hata hivyo kwa mujibu wa sheria ya makosa ya jinai, kwa kosa la matumizi mabaya ya madaraka/ofisi adhabu yake ni kulipa faini ya Sh. milioni 2 au kifungo cha kati ya mwaka mmoja au miaka mitatu jela, baada ya mshtakiwa kupatikana na hatia.

Hukumu ya watuhumiwa ambayo ilisambaa kwa muda mfupi kwenye mitandao ya jamii imetolewa na jopo la majaji watatu, ambao ni Jaji John Utamwa, Jaji Samu Rumanyika, pamoja na Hakimu Saul Kinemela kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ya jijini Dar es Salaam.

Taarifa zinasema mtuhumiwa wa tatu wa kesi hiyo, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Gray Mgonja ameachiwa huru baada ya kuonekana hana hatia. Vilio vya ndugu wa watuhumiwa vilitawala mahakamani hapo baada ya hukumu hiyo kutolewa na watuhumiwa wakipanda magari kuelekea gereza la Ukonga kwa ajili ya kuanza maisha ya gereza.

Pamoja na hayo wakili wa washtakiwa hao, Peter Swai, ameviambia vyombo vya habari kwamba hukumu hiyo haikutolewa sawa hivyo wamepanga kukata rufaa.

“Hatujaridhika na hukumu ila shauri limesikilizwa na mahakimu wa tatu. Na kwa mujibu wa sheria tukikata rufaa aidha watakubali wote watatu au mmoja wao atakataa, kwa hiyo iwapo mmoja wao atakataa na wawili wakikubaliana hiyo ndiyo hukumu ya mahakama, na hicho ndicho Mahakama ilichofanya, hili ni jambo la kisheria kama tunaamini kwamba uamuzi uliotolewa hauendani na sheria tutakata rufaa kwenye mahakama ya juu na itatafsiri sheria upya na sisi tutapata majibu,” alisisitiza wakili Swai.

Awali katika mashtaka hayo ilidaiwa kuwa washtakiwa wakiwa watumishi wa Serikali, Oktoba 10, mwaka 2003 walikaidi ushauri wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wa kuwataka wasitoe msamaha kwa Kampuni ya Alex Sterwart (Assayers) Government Business Corporation. Novemba 25, mwaka 2008, washtakiwa hao, walifikishwa katika mahakama hiyo mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Hezron Mwankenja, na kusomewa mashitaka 13, likiwamo la matumizi mabaya ya madaraka. Kesi hiyo ilipangiwa jopo hilo na kuanza kuisikilizwa mapema mwaka 2009.