Na Mwandishi wetu, Dodoma
MBUNGE wa Baraza la Wawakilishi (B.L.W) wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Mussa Khamis Silima amefiwa na mkewe baada ya gari alilokuwa akisafiri nalo kupata ajali likitokea Morogoro kuja mjini Dodoma.
Akizungumzia tukio hilo jana bungeni Dodoma, Spika Anne Makinda aliliarifu Bunge kuwa ajali hiyo iliyosababisha kifo ilitokea juzi majira ya saa 1:45 usiku eneo la Nzuguni katika Manispaa ya Dodoma.
Bunge jana lililazimika kukaa kimya kwa dakika moja likikumbuka msiba huo kabla ya kuendelea na shughuli nyingine za bunge, mara baada ya Makinda kutoa tangazo hilo bungeni.
“Waheshimiwa Wabunge naomba nitamke kwa masikitiko makubwa kuwa jana Agosti 21 saa mbili kasorobo katika eneo la Nzuguni, mheshiwa Mussa Silima akiwa na msafara na familia yake walipata ajali na katika ajali hiyo mke wa Mbunge alifariki, naomba tusimame kwa dakika moja kumkumbuka,” alisema Makinda.
Alisema Marehemu, Mwanaheri Twalib ambaye mwili wake ulisafirishwa jana kwa ndege ambayo pia ilimbeba mumewe (mbunge) na dereva wake kwa ajili ya kupelekwa jijini Dar es Salaam kwa matibabu, anatarajia kuzikwa kwao baada ya taratibu kukamilika.
Akifafanua zaidi, Makinda alisema ajali hiyo imetokea wakati mbunge huyo akitokea Zanzibar, ambako walikwenda kumzika Kaka yake na marehemu mkewe na walikuwa wakirejea kuwahi vikao vya bunge vilivyokuwa vikiendelea Dodoma.