Na Mwandishi Wetu, Dodoma
MWENYEKITI wa Bodi ya Ngorongoro, Pius Msekwa amesema tuhuma zilizotolewa bungeni na Mbunge wa Ngorongoro, Kaika Telele wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuwa alikimbia mjadala bungeni na kwenda kugawa maeneo kwa wawekezaji ya ujenzi wa hoteli ni za uongo na uzushi.
Msekwa amesema huenda mbunge huyo ameamua kumpakazia maneno hayo ya uzushi kwa chuku kwa kile, Telele kutoteuliwa kuwa Mjumbe wa Bodi hiyo tangu mwaka 2009.
Msekwa ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa CCM, Tanzania Bara alijibu mapigo hayo jana mjini hapa alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kutolea ufafanuzi juu ya tuhuma zilizoelekezwa kwake hivi karibuni.
“Naomba mnielewe maana ya neno usongombingo, si uongo wa kawaida, huu ni uongo wenye fitina ndani yake…mheshimiwa Telele ameripotiwa na magazeti mbalimbali kwamba alinizulia mimi tuhuma kwamba badala ya kuwapo bungeni wakati wa mjadala wa kupitisha Bajeti ya Maliasili na Utalii nilikwenda Ngorongoro kugawa maeneo ya kujenga mahoteli ya kitalii kwa wawekezaji,”
“Nakanusha maneno hayo kwa kutamka kwamba ni maneno ya uongo, na ukweli wake ni kwamba; mimi kama Mwenyekiti nilishahudhuria Kikao cha Kamati ya Bunge inayoshughulikia maliasili, vile vile nilikwishahudhuria Kikao cha Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma, na Ngorongoro ni Shirika la Umma, na katika kamati hizo nilipewa fursa ya kutoa maelezo pamoja na kujibu maswali ya wabunge kuhusu usimamizi unaofanywa na na bodi yangu juu ya shughuli za Mamlaka ya Ngorongoro,” alisema Msekwa.
Aidha aliongeza kuwa baada ya kazi hiyo alijipangia majukumu mengine ya kufanya kwani wakati wa mjadala wa Bunge lenyewe hakuwa na eneo la kumtaka aeleze chochote wala kujibu maswali husika.
“Pale kuna hoteli zilijengwa zamani na ilipokuja NEMC ikasitisha kujenga katika eneo hilo ,kwa hiyo majengo yaliyopo pale yote ni ya zamani.”
Hata hivyo Msekwa alipinga vikali tuhuma kwamba analitumia vibaya jina la Rais Jakaya Kikwete kwa kugawa viwanja eneo la ‘Crater rim’ sehemu isiyoruhusiwa kujengwa hoteli, alifafanua kuwa Rais Kikwete alifanya kikao na Mwenyekiti wa Bodi (Msekwa). Desemba 28, 2006, pamoja na Kaimu Mhifadhi (kabla hajateuliwa kuwa Mhifadhi) wa Ngorongoro, Bernard Murunya hotelini Ngorongoro, Serena na alipokuwa katika mapumziko ya Krismas 2006.
“Kweli akutukanaye hakuchagulii tusi, Mheshimiwa Telele amenitukana kwa kusema uongo mwingi dhidi yangu, Sijui kama fitina hizi ni chuki zake yeye binafsi zilizosababishwa na kuondolewa kwenye Ujumbe wa Bodi ya Ngorongoro, au ametumwa na watu wengine,” alisema