Na Janeth Mushi, Arusha
MLINZI wa Kampuni ya Ulinzi ya Mint Master Security, aliyefahamika kwa jina moja la Hassan anatafutwa na Jeshi la Polisi mkoani hapa kwa tuhuma za kuiibia Kampuni ya Ndege ya Precision Air zaidi ya Sh. milioni 35.193 na Dola za Marekani 7,702 ambazo ni mauzo ya tiketi ya siku mbili ya shirika hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo mjini hapa, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Ibrahim Kilongo alisema tukio hilo lilitokea juzi usiku eneo la Goliondoi Sekei wilayani Arumeru kwenye ofisi za kampuni ya Precision.
Alisema fedha hizo ni mauzo ya tiketi ya Ijumaa na Jumamosi. Amesema mlinzi mwenzake, Peter Edward (23) ndiye aliyeshtukia tukio hilo baada kwenda kupokea zamu Jumapili saa 2:00 asubuhi, ambapo hakumkuta na KUgundua sanduku la kuhifadhia fedha lililokuwa ofisini hapo limevunjwa.
Kakamnda alisema baada ya kugundua alitoa taarifa polisi na walipofika eneo hilo walikuta sanduku hilo limevunjwa na kukuta ujumbe wa karatasi aliyouacha, Hassan kuwa asitafuwe kwa madai kuwa amekwenda Dar es Salaam.
Alisema pia walikuta nyaya za camera ya CCTV zimekatwa ili zisioneshe picha halisi ya tukio hilo lakini polisi wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo.
Aidha katika tukio lingine watu wanne wanashikiliwa kwa kukutwa na nyaraka za Serikali ambazo ni mihuri ya Ofisa Biashara wa Jiji la Arusha, Leseni ya kuendeshea biashara daraja ‘A’, pamoja na kadi ya usajili wa magari namba 2425794.
Alisema watuhumiwa hao walikutwa na leseni tatu za magari ambazo ni 3465990, 4265914 na 03349158. Aliongeza watuhumiwa hao walikamatwa majira ya mchana katika Ofisi za Makao Makuu ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoani Arusha.
Aliwataja watuhumiwa hao ni Hamis Athumani (35), John Fayu(43), Lucas John (50) na George Foroma (51). Wakati huo huo, Polisi inawashikilia, Hussein Hamis (43) na Prosper Thomas (35) kwa tuhuma za kupora gari aina ya Nissan Pickup namba T386 AHX mali ya Shirika lisilo la kiserkali la Kilimanjaro Cooking.
Kamanda Kilongo amesema watuhumiwa hao wanadaiwa kuliiba gari hilo eneo la Ngarenaro nyumbani kwa dereva wake, Athur Mallya (26) ambaye ni Mhasibu wa shirika hilo na baadaye kukutwa katika baa ya Club Afrikano iliyopo Usa River wilayani Arumeru.
Watuhumiwa hao walipopekuliwa walikutwa na bastola aina ya Browing yenye namba ‘A’ 8022 ikiwa na risasi moja iliyotengenezwa Slovakia.