AJAAT, TACAIDS kuwashindanisha waandishi habari za Ukimwi

Mwenyekiti wa AJAAT, Simon Kivamwo akizungumza leo jijini Dar es salam na waandishi wa habari kuhusu kuanza kwa shindano la kuandika makala juu ya upatikanaji wa huduma za UKIMWI kwa makundi ya watu walionyimwa fursa na wale wanaoishi katika mazingira hatarishi kwa maambukizi ya VVU. (Picha na Tiganya Vincent- MAELEZO-Dar es Salaam)

Na Esther Muze na Tiganya Vincent, MAELEZO- Dar es Salaam

CHAMA cha Waandishi wa Habari za UKIMWI (AJAAT) kwa kushirikiana na Tume ya Kudhibiti UKIMWI nchini (TACAIDS) kimeanzisha shindano la miezi mitatu la uandishi wa makala za UKIMWI kwa mwaka 2011.

Akitoa maelezo kwa waandishi wa habari leo mjini hapa, Mwenyekiti wa AJAAT, Simon Kivamwo amesema kuwa washiriki wa shindano hilo wanapaswa kuandika makala juu ya upatikanaji wa huduma za UKIMWI kwa makundi ya watu walionyimwa fursa na wale wanaoishi katika mazingira hatarishi kwa maambukizi ya VVU.

Alisema lengo la shindano hilo ni kuwahamasisha waandishi wa habari kuandika kwa mapana juu ya uhusiano ulipo kati ya upatikanaji huduma za VVU kwa wanaoishi katika mazingira hatarishi kwa upande mmoja na uwezekano wa kuongezeka kwa maambukizi ya VVU endapo watu hawa watanyimwa huduma hizi kwa upande mwingine.

Kivamwo alisema makundi yanayolengwa ni yale yanaoendesha biashara ya ngono, watu wenye ulemavu, ombaomba, wafungwa, mashoga, na watumiaji wa dawa za kulevya.

“Wakati huduma za UKIMWI zinaongezeka katika baadhi ya vitengo, makundi ya waliomo katika mazingira hatarishi ya kuambukizwa UKIMWI yanazidi kupambana na vikwazo vya kiufundi, kisheria na vya kiutamaduni katika kupata huduma ya matunzo ya kiafya,” alisema Mwenyekiti huyo.

Alisema kuwa ili kuibuka na makala zinazojitoshereza waandishi wa habari wanatakiwa kuaandaa, vipindi au picha zinazoandika kwa undani na kuibua changamoto za kisera, na mipango ya Serikali na mamlaka zake katika tatizo la UKIMWI.

Kivamwo aliongeza kuwa waandishi wa habari wanapaswa kuonesha udhaifu (kama upo) katika Sera na athari za jamii kwa makundi yaliyo katika mazingira hatarishi endapo watakuwa hawapati huduma za VVU na kushauri mwelekeo sahihi na bora katika mapambano ya UKIMWI.

Pamoja ya hayo waandishi katika makala yao wanatakiwa kuonyesha maoni na ushauri wa sekta binafsi kuhusiana na upatikanaji wa huduma za UKIMWI kwa wote walio katika mazingira hatarishi kama njia mbadala wa kupunguza maambukizi ya VVU.

Kivamwo alisema kuwa shindano hilo liloanza Agosti 22, 2011 na linatarajiwa kuhitimishwa siku ya kilele cha Siku ya UKIMWI Duniani Desemba Mosi, 2011 na linawashirikisha wandishi wa habari wa magazeti, majarida, vituo vya runinga, redio, wachora vikaragozi na mitandao ya blogu.

Alisema kuwa jumla ya washindi 15 watazawadiwa ambapo viwango vya juu vitakuwa shingi 700,000/- na kiwango cha chini ni 300,000/-.