Na Mwandishi Wetu
SHIRIKA la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) linatoa huduma za afya bure kwa wateja mbalimbali watakaotembelea katika Banda la shirika hilo ndani ya Maonesho ya 39 ya Kimataifa ya Biashara, Sabasaba yanayofanyika viwanja vya Mwalimu Julias Nyerere Barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi leo Dar es Salaam ndani ya banda la NSSF Sabasaba, Ofisa Mwandamizi wa Mafao ya Matibabu, Dk. Straton Simon alisema shirika hilo limeamua kutoa huduma bure kwa wateja mbalimbali watakaowatembelea katika banda lao kwa muda wote wa maonesho hayo ili wajue afya zao na kupata ushauri kwa madaktari.
Dk. Simon alisema wameamua kutoa huduma za afya bure kwa magonjwa ambayo si ya kuambukiza na hayakupewa kipaumbele na Serikali kama ilivyo kwa magonjwa mengine ikiwa ni mkakati wa kuhamasisha jamii kupenda kupima na kujua afya zao mara kwa mara. Aliongeza kuwa NSSF imeleta wataalamu wa vipimo pamoja na madaktari ambao wanaendesha zoezi hilo kwa wateja wanaowatembelea katika banda lao.
Alisema miongoni mwa vipimo ambavyo vinatolewa huduma ni pamoja na kuangalia shinikizo la damu (presha), kuangalia ugonjwa wa kisukari na kuangalia uwiano wa uzito na urefu kwa mteja kisha kupata nafasi ya kuonana na daktari moja kwa moja kujua matatizo ya mteja na kupata ushauri wa kitabibu na pia kuelezwa nini cha kufanya.
“…Tumeona ni vema kwenye kipindi hiki cha sabasaba tuweke huduma za afya ili kupima watu wote watakaopita kwenye banda hili…kuangalia urefu na uzito, baadaye tutapima presha yao, na sukari na hatimaye tunatoa ushauri kwa mteja juu ya nini cha kufanya na kama atakuwa na matatizo tunamuelekeza nini cha kufanya au pa kwenda kulingana na matatizo yake,” alisema Dk. Simona katika ufafanuzi wake.
Aidha alisema NSSF ambayo pia inatoa fao la matibabu imeleta wataalamu wa vipimo pamoja na madaktari wawili kushirikiana kuendesha zoezi hilo la kutoa huduma za afya bure kwa wananchi wanaotembelea banda la Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii katika viwanja hivyo vya maonesho ya kimataifa ya biashara.
Hata hivyo aliwataka wananchi wanaotembelea viwanja hivyo kupita katika banda la NSSF ili kujua afya zao na pia kupata ushauri wa madaktari. “…Tunapima watu wote wanaotembelea katika banda letu awe mwana chama au sio mwana chama, na umri kuanzia miaka 18 na kuendelea…tupende kupima afya zetu inasaidia kujua hali yako na kutatua tatizo mapema kama unalo, waweza kuwa unatembea lakini hujui unatatizo la kiafya sasa ukija hapa utaangaliwa,” alisema.
Kwa upande wake Meneja Kiongozi Masoko na Ushirikiano wa, Bi. Eunice Chiume aliwakaribisha wanachama wote wa NSSF na wasio kujionea na kupata huduma mbalimbali zikiwemo, taarifa za jumla zinazohusu kujiandikisha uanachama, uwekezaji unaofanywa na Shirika, maelezo zaidi kuhusu Bima ya afya itolewayo na NSSF na huduma za kadi mpya.
“Wageni wote wanaotutembelea wanaweza kujua kuwasilisha maoni yao kupitia mfumo wetu mypa wa HaapyOrNot uliopo katika ofisi za Kinondoni, Ilala, Temeke na GDE- Waterfront Kwa kutumia mfumo huo mwanachama na asiye mwanachama anaweza kutuambia amefurahia huduma au Hapana pindi anapotembelea Ofisi za NSSF. Pia wastaafu wote wanaofaidika na Pensheni za NSSF wataweza kupata pensheni kupitia mfumo mpya wa HIFADHI SMART ambapo mstaafu ataweza kupata fedha zake sehemu yoyote,” aliongeza Bi. Chiume.