MAAJABU yametokea Mjini Bagamoyo baada ya mtu aliyefahamika kwa jina moja, Bi. Hatujuani kuzinduka na kuanza kupumua wakati maiti yake ikioshwa tayari kwa kuzikwa. Tukio hilo limetokea eneo la Majani Mapana jana baada ya mwanamama huyo kufia hospitalini tarehe 28 na daktari kuthibitisha na msiba kuanza nyumbani kwa wanafamilia huku taratibu za mazishi zikifanywa ili azikwe.
Hata hivyo tarehe 29 mwanamama huyo aliyezua tafrani alizinduka akiwa anaoshwa na kuanza kupumua jambo ambalo liliwashangaza wengi na msiba kufutwa japokuwa waombolezaji waligoma kuondoka wakitaka ufafanuzi wa kutosha wa tukio hilo.
“…Bi. Hatujuani aliugua kwa muda na kukimbizwa hospitali ya Wilaya Bagamoyo baadaye kufia hospitalini hapo na hospitali kuthibitisha kuwa keshakufa, msiba ukatangazwa turubai likafungwa, sanda ikaandaliwa lakini Juni 29, 2015 wakimkosha walishtuka maiti kuwa anajoto kali, anatoka jasho na anakunja na kukunjua mikono na miguu…lakini kusema wala kusimama hawezi,” alisema shuhuda mmoja.
Alisema baada ya kioja hicho wanandugu waliingia tafrani na kutangaza hakuna tena msiba na kushushwa turubai kisha kueleza kilichopo ni mgonjwa maututi. Hata hivyo waombolezaji waligoma kuondoka msibani hapo wakidai hadi kieleweke nini kilitokea?