Stars Yawasili Zanzibar

zanzibar

Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) inayodhaminiwa na bia ya Kilimanjaro Premium Lager, imewasili leo asubuhi Visiwani Zanzibar tayari kwa maandalizi ya mchezo wa siku ya jumamosi dhidi ya timu ya Uganda kuwania kufuzu kwa CHAN 2016.

Msafara wa Taifa Stars unajumuisha wachezaji 21 na benchi la ufundi 7 ambao wamefikia katika hoteli ya Nungwi Inn, mchezo dhid ya Uganda utachezwa katika uwanja wa Amani kisiwani Zanzibar jumamosi kuanzia majira ya saa 2 usiku.

Stars inakutana na Uganda katika mchezo huo wa awali wa kuwania kufuzu kwa fainali za mataifa Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN) zitakazofanyika mwakani nchini Rwanda, kabla ya kurudiana wiki mbili baadae katika uwanja wa Namboole jijini Kampala.

Mara baada ya kurejea kutoka nchini Misri kikosi cha Stars kiliendelea na kambi katika hoteli ya Tansoma na kufanya mazoezi katika uwanja wa Karume kabla ya kuondoka leo asubuhi kuelekea visiwani Zanzibar.

Kocha mkuu wa Taifa Stars, Mart Nooij amewaongeza wachezaji watano ambao hawakua katika kikosi kilichocheza dhidi ya Misri, kufuatia wachezaji wa kimataifa wa Tanzania kutoruhusiwa kucheza mchezo huo wa CHAN wikiendi hii.

Wachezaji waliongezwa ni Atupele Green, Hassan Isihaka, Hassan Dilunga, Rashid Mandawa na Kelvin Friday, wanaungana na wachezaji Deogratias Munish, Mwadini Ali, Shomary Kapombe, Oscar Joshua, Salum Mbonde, Aggrey Morris na Nadir Haroub.

Wengine ni Jonas Mkude, Erasto Nyoni, Mwinyi Haji, Abdi Banda, Frank Domayo, Amri Kiemba, Said Ndemla, Saimon Msuva, na John Bocco.

Aidha Shirikisho la Mpirani wa Miguu barani Afrika (CAF) limetoa mwongozo kuwa mchezaji Mrisho Halfan Ngasa haruhusiwi kucheza CHAN kwa sababu sio mchezaji tena wa ndani, hivyo Ngasa ameondolewa kikosini

Waaamuzi wa mchezo huo wanatarajiwa kuwasili kesho kutoka nchini ambao ni Hudu Munyemana (Rwanda), akisaidiwa na Hakizimana Ambroise (Rwanda), Justin Karangwa (Rwanda), mwamuzi wa akiba ni Issa Kagabo (Rwanda), na kamishina wa mchezo Nicholaus Musonye kutoka Kenya.

U15 KUINGIA KAMBINI JUMATATU
Kikosi cha timu ya Taifa ya vijana umri chini ya miaka 15 (U-15) kitaingia kambini siku ya jumatatu tarehe 22/06/2015 ili kujiandaa na mchezo wa kirafiki dhidi ya kombaini ya mkoa wa Mbeya, mchezo utakaofanyika mjini Mbeya jumatatu ya tarehe 28/06/2015.

Kikosi hiki kinaandaliwa kwa ajili ya kujiandaa na na michuano ya mtoano kuwania kufuzu kwa fainali za Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka 17 zitakazofanyia nchini Madagascar mwaka 2017. Hatua ya mtoano wa awali itaanza mwakani 2016 mwezi Juni.

Timu itakua chini ya kocha Bakari Shime kwa muda akisaidiwa na Peter Manyika. Kocha aliyekua ameteuliwa awali kufundisha timu hiyo Adolf Rishard ameomba udhuru baada ya kupata fursa ya kwenda masomoni.

Wachezaji watakaoingia kambini na mikoa wanayotokea kwenye mabano ni Mwijuma Yahya (Tanga), David Mpakazi, Shilole Anthony (Geita), Kibwana Shomari , Ibrahim Koba, (Morogoro), Faraji John, Kelvin Deogratius, Davison Meddy , Maulid Lembe (Dodoma), Ally Msengi (Mwanza).

Wengine ni Timoth Timothy, Juma Juma, Pius Raphael, Mohamed Ally (Dodoma), Athumani Rajabu, Juma Zubeir, Jonathan Rafael (Kigoma), Robert Philip, Jaffari Juma (Arusha), Michael Kanuti, Alex Peter, Rashid Kilongola (Kinondoni), Morris Michael (Ilala), Karim Mfaume (Lindi), Assad Juma (Unguja Magharibi), Francis Mrope, Kelvin Pius (Mara)