Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa binafsi hana mgombea Urais ambaye anampendelea kwa sababu wagombea wote ni wa kwake na wa chama chake, isipokuwa anayo kura moja tu ambayo ataitumia mwezi ujao wakati wa vikao mbalimbali kuamua nani awe mgombea Urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM) katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu, 2015.
Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa hana tatizo na kujitokeza kwa wagombea wengi wa nafasi ya Urais zamu hii kupitia CCM kwa sababu huwezi kuwazuia watu kugombea nafasi hiyo kwa sababu ni haki yao.
Vile vile, Rais Kikwete amesema kuwa wingi wa wagombea zamu hii ni jambo zuri na ni ushahidi wa kiasi cha uhuru ambao umejengeka katika chama hicho na uthibitisho kuwa uongozi wa Tanzania katika miaka 10 iliyopita umekuwa wa mafanikio.
Rais Kikwete amesema hayo usiku wa kuamkia jana, Jumatatu, Juni 14, 2015 mjini Johannesburg, Afrika Kusini wakati anazungumza na Waziri Mdogo wa Mambo ya Nje wa Marekani anayeongoza Kitengo cha Masuala ya Afrika Bi. Linda Thomas-Greenfield.
Viongozi hao wawili walikuwa wanahudhuria Mkutano wa 25 wa Kawaida wa Nchi Wanachama wa Umoja wa Afrika kwenye Kituo cha Mikutano cha Sandton Covention Centre, Johannesburg, Afrika Kusini uliomalizika jana.
Mwanzoni tu mwa mazungumzo hayo, Bi. Lidsey alimwuliza Rais Kikwete: “Mheshimiwa Rais, je unaye mgombea yoyote ambaye unampendelea miongoni mwa utiriri wa wagombea?”
Rais Kikwete alimjibu: “Sina mgombea ninayempendelea, wagombea wote ni wa kwangu, ni wa Chama changu, isipokuwa ninayo kura moja ambayo kwa mujibu wa taratibu za haki katika Chama chetu nitaitumia katika vikao mbali mbali.”
Kuhusu kile kinachoitwa utiriri wa wagombea, Rais Kikwete amesema kuwa wingi wa wagombea ni jambo zuri kwa CCM. “Hiki ni chama kikubwa. Wingi unatupa nafasi ya kujadili kwa nafasi nani awe mgombea wetu. Isitoshe, tunaona wagombea wengi zamu hii kwa sababu ya wigo mkubwa wa uhuru ambao umejengeka katika nchi yetu katika miaka ya karibuni. Vile vile, wingi wa wagombea unathibitisha mafanikio yetu katika miaka 10 iliyopita kwa sababu tungeshindwa, watu wangeogopa kujitokeza kugombea nafasi hiyo.”