Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe , amenusurika kifo baada ya ndege aliyokuwa akisafiria kutoka Iringa kwenda Zanzibar kutaka kugongana uso kwa uso na ndege nyingine ikiwa inadakika moja kabla ya kutua.
Waziri Membe akiwa na ujumbe wake wa watu wanane, walikuwa wakisafiria ndege ya kukodi ya kampuni ya 5H NEG Precision Aviation ikirushwa na rubani Mathew Mhahiki, ambaye ameonyesha kushangazwa na tukio hilo alilodai “ni kwa rehema za Mungu tumepona ajali hii.”
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, rubani Mhahiki alisema: “Lazima kuna tatizo katika control center hata hivyo tayari nimeongea nao na wameniomba samahani na kudai walipitiwa, maana kwa hali ilivyokuwa ni kwamba tungegongana wakati wa kutua maana nimeshangaa tu kuona ndege hii hapa ndiyo maana nikaamua kumkwepa mwenzangu nikapanda juu.”
Waziri Membe alisema: “Nina uzoefu mkubwa wa kusafiri na ndege mahali pengi duniani, hali hii ilikuwa ni ajali na labda sasa tungekuwa dead bodies, lakini ninajua Mungu yuko upande wetu katika safari hii ya uhakika, lakini pia izingatiwe nimekuja kufanya kazi ya Mungu.”
“Katika safari hii tutashuhudia mambo mengi sana, lakini kwa kuwa kila ninapotaka kuondoka nyumbani ama hotelini mara nyingi nimekuwa nikimtanguliza Mungu maana bila Mungu hii ilikuwa ni mwisho wa maisha yetu tuliokuwa kwenye ndege hii.”
Waziri Membe alikuwa amealikwa mjini hapa na Umoja wa Akinamama wa Kikristu (Umaki) wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Zanzibar waliokuwa wakifanya mkutano wao mkuu unaofanyika kila baada ya miaka mitano akitokea Iringa ambako alikwenda kutafuta udhamini wa chama ili kumwezesha kugombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi, CCM.
Akiwa katika mkutano huo, Waziri Membe alisema: “Miongoni mwa mambo yanayonikera ndani nafsi yangu ni kuona mwanamke bado anaachwa nyuma, hili halipendezi, ni lazima tuhakikishe wanawake wanapata elimu ya ufundi stadi maana mwanamke akiwezeshwa hasa katika eneo hili la elimu wanaweza hata kushinda wanaume wengi.”
“Ni lazima kina mama wawezeshwe kujiajiri ili msiwategemee kina baba kwa kila jambo lakini pia ili kufikia malengo hayo ni lazima tuwape elimu kina mama.”