Na Mwandishi Wetu, Mwanza
JESHI la Polisi mkoani Mwanza linawashikilia Scolastica Juma (25) na Nyambura Wambura (24) kwa tuhuma za kumuua mwanafunzi wa Shule ya Msingi Sokoine, Martha Thobias (8) kwa madai alikutwa akikomba mboga.
Watuhumiwa Scolastica ambaye ni mama mzazi wa marehemu huku Nyambura Wambura akiwa ni mfanyakazi wa ndani wanadaiwa kumshambulia kwa zamu kwa kutumia fimbo mtoto Martha Thobias hadi kusababisha kifo chake, baada ya kumkuta akikomba mboga.
Akizungumzia tukio hilo jana Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Liberatus Barlow alisema, polisi inawashikilia watuhumiwa hao baada ya kusababisha kifo cha mtoto huyo, waliyekuwa wakiishi naye.
Kamanda alisema watuhumiwa wanadaiwa kufanya kitendo hicho, Agosti 18 mwaka huu, majira ya saa 8:00 mchana, Bugarika huku chanzo kikidaiwa kumkuta marehemu akikomba mboga, ndipo walipoanza kumshambuliwa, hadi alipofikwa na mauti.
Hata hivyo Kamanda Barlow alisema watuhumiwa wote wako mahabusu, na Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wa tukio zima ndipo liwafikishe mahakamani watuhumiwa kukabiliana na kesi yao.
Akifafanua alisema kitendo hicho ni cha kinyama na ukiukaji wa haki za binadamu tena kufanywa na mtu ambaye ni mzazi wa marehemu. “…Ni cha kinyama hakistahili kufanywa na mzazi ama jamii, kwani huu ni ukiukwaji wa sheria na haki za binadamu, kwa sababu kila binadamu anayo haki ya kuzaliwa na kuishi,” alisema Kamanda Barlow.